Heade

WAZIRI MKUU MAJALIWA AAGIZA DED AELEZE SHILINGI MILIONI 350 ZILIPO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Frank Bahati aeleze amepeleka wapi zaidi ya Sh milioni 350 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi.
Ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Waziri Mkuu amesema serikali haiwezi kuvumilia kuona fedha inazopeleka katika halmashauri hiyo kwa ajili ya kugharamia miradi na kulipa madai ya watumishi, zinatumika kinyume na maelekezo.
Amesema, miongoni mwa fedha hizo ni Sh milioni 451.47 za miradi ya maendeleo (CDG), ambapo zilizotumika ni Sh milioni 221.9 tu.
" Namtaka Mkurugenzi na Mweka Hazina wa halmashauri hii, Peter Mollel tarehe 21 mwezi huu, waje Mwanza wanieleze walikopeleka fedha hizo," amesema.
Waziri Mkuu amesema, fedha nyingine ni Sh milioni 50 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kulipa madai mbalimbali ya watumishi kama likizo, ambapo zililipwa Sh milioni 13 na nyingine hazijulikani zilipo.
Pia serikali ilitoa Sh milioni 65 za kugharamia mradi wa umwagiliaji wa Bugorola, ambazo nazo hazijulikani zilipo pamoja na Sh milioni 84 zilizotolewa kwa ajili ya kulipa motisha kwa walimu, ambapo zilizolipwa ni Sh milioni 60 tu.
Alisema, "Kama mlidhani Ukerewe ni sehemu ya kutafunia fedha za umma mmekosea, kwa sababu Serikali haiwezi kuvumilia haya, Mkurugenzi umeaminika na kupewa dhamana ya kusimamia rasilimali za umma lakini unafanya tofauti."
Majaliwa alisisitiza kwamba lazima viongozi hao, wahakikishe fedha zinazopelekwa na Serikali katika halmashauri zao zikiwemo za utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, uvuvi zinatumika kama ilivyoelekezwa na si vinginevyo.
Pia Waziri Mkuu alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, asimamie utendaji wa viongozi na watumishi katika wilaya zote za mkoa huo na kisha kutoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, John Mongella.

No comments

Powered by Blogger.