MFANYABIASHARA Gairo Mtozoma (43) amehukumiwa kifungo cha miaka 10
jela katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukutwa na hatia ya
mashitaka mawili ya kupatikana na silaha na risasi.
Mtozoma ambaye pia ni mkazi wa Magomeni Kagera, alihukumiwa kifungo hicho jana mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.
Hakimu Mwambapa alisema kuwa upande wa mashitaka, ulikuwa na
mashahidi watano kwa ajili ya kuthibitisha mashitaka hayo na kwamba
baada ya kusikiliza ushahidi huo, mahakama ilimuona mshitakiwa kuwa na
kesi ya kujibu na kujitetea mwenyewe.
Alisema katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, mashitaka ya kwanza ya
kupatikana na silaha, mshitakiwa huyo atatakiwa kutumikia kifungo cha
miaka mitano jela na katika mashitaka ya pili atatumikia kifungo cha
miaka mitano. Kabla ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Nassoro Katuga aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa
mshitakiwa iwe fundisho kwa wengine.
Katika kesi ya msingi, inadaiwa Agosti 11, mwaka jana maeneo ya
Magomeni Kagera wilayani Kinondoni, Mtozoma alikutwa na bastola moja
aina ya Browing yenye kumbukumbu namba 90002 iliyosajiliwa kwa namba
TZCAR-A222683 bila kuwa na leseni.
Pia inadaiwa Agosti 11, mwaka jana maeneo ya Magomeni Kagera wilayani Kinondoni alikutwa na risasi sita bila kuwa na leseni.
No comments