WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali haitawavumilia wote,
wanaotumia vibaya fedha za serikali, ambazo zinapaswa kuleta maendeleo
kwa wananchi zikiwemo za Mfuko wa Udhibiti Ukimwi.
Majaliwa alisema Dar es Salaam jana wakati akifungua kongamano la
Kitaifa la Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani 2017, kaulimbiu ikiwa
‘Changia Mfuko wa Udhamini wa Udhibiti Ukimwi, Okoa Maisha.”
Alisema wito wake ni kuhakikisha bodi ya mfuko huo, inasimamia vizuri
fedha hizo zinazochangiwa na wadau mbalimbali ili kuwahakikishia
usalama wake. “Fedha hizi zikitumika vinginevyo hatutavumiliana. Malengo
ni kuhakikisha fedha hizo zinazotolewa na wadau zinatumika kama ambavyo
imekusudiwa,” alisema Majaliwa.
Alisema anayo furaha kuwa Mfuko huo wa Udhibiti Ukimwi umeanza
kufanya kazi, ambapo Oktoba 21, mwaka huu kwa mara ya kwanza Mfuko huo
uligawa fedha kwa ajili ya shughuli za kudhibiti ukimwi nchini Sh.
milioni 660, zilitolewa kwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kununua dawa za
Cotrimoxazole ambazo hutumika kutibu na kuzuia magonjwa nyemelezi kwa
watu waishio na virusi vya Ukimwi.
Alisema serikali itaendelea kutenga fedha za mfuko huo na kuhakikisha
inahamasisha wananchi na wadau, ikiwemo sekta binafsi kuchangia mfuko
huo muhimu. Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga
Tanzania ya viwanda na ili ifikie lengo hilo ni lazima wananchi wawe na
afya bora.
“Nguvu kazi kwa ajili Tanzania ya viwanda itatokana na wananchi wenye
nguvu na afya bora. Hivyo serikali tutahakikisha tunaendelea kutoa
huduma bora za afya ili wananchi wetu waweze kuwa na afya bora,”
alisema.
Alisema watu milioni 16 ya Watanzania wote ni vijana na wanapaswa
kukingwa dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Ukimwi ili taifa liwe na
nguvu kazi ya kutosha hasa kipindi hiki linapoanza mageuzi makubwa ya
kiuchumi na kimaendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids),
Dk Leonard Maboko alisema kongamano hilo ni sehemu ya shughuli za
Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani, itakayofanyika Desemba mosi hapa
nchini.
Alisema maonesho ya maandalizi hayo yalianza Jumamosi, yakijumuisha
huduma mbalimbali za utoaji elimu na burudani kwa wananchi ikiwemo
ushauri nasaha na upimaji wa hiari wa VVU.
Alisema pia kuwa tayari wamezindua mkakati wa kitaifa wa kondomu wa
miaka mitatu wa 2016 hadi 2018, na siku ya kilele cha maadhimisho hayo
kutakuwa na uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Kitaifa wa Matokeo ya
Ukimwi wa Mwaka 2016/17.
No comments