MWANAMKE ambaye yupo kwenye ndoa kwa miaka 55, amefungua kesi
mahakamani kuomba mumewe ampe talaka kwa madai kuwa hamjali, na
anamthamini zaidi mke mdogo.
Mwalimu huyo mstaafu, Marcella Mukami Kinyugo (73), anaiomba Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kangema, isitishe ndoa yake na Peter Kinyugo (76)
iliyofungwa Septemba 16, 1962 katika Kanisa Katoliki Kiriaini.
Bibi huyo mkazi wa mjini Kiria-ini, Mathioya, kwenye kaunti ya
Murang’a, pia aliomba apewe nusu ya mali za familia yao na pia mumewe
alazimishwe kulipa gharama za kesi. Katika kesi hiyo bibi huyo
aliwakilishwa na Margret Nyangati kutoka kampuni ya mawakili ya Muchoki
Kang’ata.
Aliieleza Mahakama kuwa, waliishi maisha ya furaha ya mume na mke
tangu walipofunga ndoa, lakini miaka sita iliyopita hali ilibadilika
wakati mumewe alipoacha kutimiza majukumu yake kama mume.
Mume wa bibi huyo ni mwalimu mstaafu na Chifu. Mukami alidai
mahakamani kuwa matatizo yalianza baada ya Kinyugo kukaa kwa mke mdogo
kwa wiki kadhaa bila kwenda kwake, na kwamba, yeye na mke mwenzake
wanaishi kwenye eneo moja. Kwa mujibu wa bibi huyo, wakati mumewe
anafanya hivyo, hawakuwa na ugomvi.
No comments