KATIKA kuendeleza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii nchini,
mabalozi tisa kati yao wanane Watanzania na mmoja Balozi wa Algeria
nchini Qatar, wanapanda mlima Kilimanjaro leo, ikiwa ni sehemu ya
jitihada za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika kuvitangaza vivutio vya
nchi yetu, ukiwemo Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, Ofisa Habari Mkuu wa
TTB, Geoffrey Tengeneza alisema wameandaa ziara hiyo ya mabalozi kwa
lengo la kuwajengea uwezo na wigo mpana wa kuvitangaza vivutio vya
utalii katika nchi watakazokwenda kuhudumia kama mabalozi. “Maandalizi
yamekamilika na tunatarajia mabalozi na wafanyakazi wa Bodi ya Utalii na
mjumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na waandishi wa kutoka Clouds
Media Group watapanda mlima Kilimanjaro kesho (leo),” alisema Tengeneza.
Mabalozi hao wanaopanda Mlima Kilimanjaro leo ni Balozi Aziz Mlima,
Balozi Samwel Shelukindo, Balozi Luteni Jenerali Wynjones Kisamba,
Balozi Pastor Ngaiza, Balozi Bernard Achiula, Balozi Alan Mzengi na
Balozi Antony Cheche. Pia yumo Balozi wa Algeria nchini Qatar, Abdelaziz
Sebaa.
Tengeneza alisema katika kupanda mlima huo mrefu kuliko wote barani
Afrika, kuna vivutio vingi watakutana navyo hivyo kuwafanya kuwa na vitu
vingi vya kusimulia kama vielelezo watakapokuwa katika maeneo yao ya
kazi na kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii ukiwemo Mlima
Kilimanjaro kwa vitendo.
“Ni matumaini yetu kuwa watakwenda kuitangaza Tanzania pamoja na
vivutio vyake katika nchi za nje na kufanya ongezeko la watalii kuja
nchini kuongeza maradufu,” alifafanua Tengeneza. Alisema kupitia ziara
hiyo, mabalozi watakwenda kutekeleza kwa vitendo Diplomasia ya Uchumi
kwa kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na ukarimu wa
Watanzania kwa wageni.
“Kama Bodi ya Utalii tunatoa wito kwa mabalozi wengine
wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi nyingine duniani kutumia nafasi
hiyo katika kuvitangaza vivutio hasa Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima
mrefu barani Afrika,” alieleza ofisa huyo wa TTB.
Kwa upande wake, Balozi wa Algeria nchini Qatar, Abdelaziz Sebaa
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi nchini humo, alisema hiyo ni nafasi
ya pekee kwake kupanda Mlima Kilimanjaro na kujionea vivutio vingine
vya utalii Tanzania.
Alisema kwa nafasi hiyo na vitu atakavyokwenda kuviona, atakwenda
kuwahamasisha mabalozi wengine katika umoja wao ili kuvitangaza vivutio
vilivyopo Tanzania, hivyo kusaidia kujenga uhusiano mzuri zaidi katika
sekta ya utalii. Ziara hiyo ya mabalozi kupanda Mlima Kilimanjaro,
imeratibiwa na TTB na katika kupanda mlima huo, wataongozwa na Kampuni
ya ZARA Tours iliyopo mjini Moshi.
No comments