MRATIBU WA MRADI WA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA WILAYANI TARIME ROSELYNE MOSAMA AKUTANA NA WADAU
Wadau kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, mashirika ,serikali na taasisi binafsi wamekutana kujadidili namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia katika wilaya ya Tarime.
Akizungumza mratibu wa mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia wilayani Tarime Roselyne Mosama amesema kwa mara ya kwanza mradi umefanikiwa kukutana na wadau kutoka maeneo mbalimbali kujadili kwa pamoja, kutafuta na kubuni mbinu mbalimbali zitazotumiwa katika harakati za kupambana na vitendo vya kikatili vinavyo waathiri watu wengi kimwili, kisaikolojia na kiuchumi suala linalorudisha nyuma maendeleo ya jamii husika na Taifa kwa ujumla.
Amesema mradi una malengo ya kuifikia jamii kwa kiwango kikubwa kutoa elimu kupitia mikutano, makongamano, matamasha,vitabu,vipeperushi na vilabu vya wanafunzi katika shule zilizopo wilayani Tarime ili jamii ipate elimu ya kutosha itakayoisaidia kubadilika na kuziacha mila kandamizi na zenye madhara makubwa ikiwemo ukeketaji na vipigo kwa akina mama na mashambulio ya aibu.
Aidha amesema mradi umewafikia watu 1500 ambao ni jamii na katika shule,watoto wa kike 550 na wa kiume 420 wamefikiwa ikiwa ni pamoja na kuunda vikundi vya maigizo,ngoma na timu za mpira wa miguu na mikono kwa wasichana mambo ambayo yatasaidia kuwakusanya vijana pamoja kuwapa hamasana na kurahisisha mpenyo wa elimu juu ya kuelewa na kupiga vita mila zilizopitwa na wakati, kandamizi na zenye athari kubwa ikiwemo ukeketaji.
Mradi huo wenye kauli mbiu inayosema"Ukatili wa Kijinsia ni Adui wa Maendeleo" umezifikia kata 9 wilayani Tarime na umekuwa chachu ya mabadiliko kwa jamii suala linaloleta matumaini ya kubadili fikra na mitazamo duni inayochochea kuwepo kwa mila zinazoiathiri jamii kimwili, kisaikolojia na kiuchumi huku zikichangia sehemu kubwa ya ongezeko la hali duni ya maisha katika jamii.
No comments