VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WASHIRIKISHWA KATIKA MAAMUZI
MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage
amewataka wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi nchini kuwashirikisha
viongozi wa vyama vya siasa katika maamuzi yenye maslahi ya pande zote ili
kuendeleza amani na utulivu nchini.
Akizungumza na wasimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro,
Jaji Kaijage amesema katika kipindi hiki ambacho vyama vinashiriki kampeni za
Uchaguzi Mdogo wa Udiwani Jumapili hii, ni muhimu wasimamizi wa uchaguzi
kuhakikisha maadili ya uchaguzi wakati wa kampeni yanazingatiwa ili kuepusha
uvunjifu wa amani miongoni mwa wananchi.
Jaji Kaijage ambaye yuko katika ziara ya kutembelea mikoa ya Tanga,
Kilimanjaro na Arusha kushuhudia utekelezaji wa Maadili ya Uchaguzi katika
Kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Udiwani, aliwataka wasimamizi wa uchaguzi
kuhakikisha vifaa vyote ambavyo vinahitajika ili uchaguzi ufanyike vimepatikana
na vile ambavyo havijapatikana wawasiliane na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kasoro
zinazobainika zipatiwe ufumbuzi kabla ya siku ya uchaguzi.
No comments