WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amebaini mpango wa kutaka kuyatoa
bandarini matrela 44 ya malori makubwa, maarufu kama semitrela, bila ya
kuyalipia kodi, huku wahusika wa mpango huo wakitumia jina la Waziri
Mkuu.
Alibaini hayo alipofanya ziara ya kushitukiza katika Bandari ya Dar
es Salaam, jana. Kutokana na tukio hilo, Majaliwa alimuagiza Mkuu wa
Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, kuwakamata mmiliki
wa kampuni ya NAS Haulage aliyetajwa kwa jina moja la Bahman na Wakala
wa Kampuni ya Wallmark, aliyetajwa pia kwa jina moja la Samwel kwa
kuhusishwa na njama hizo.
Pia Waziri Mkuu aliitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza
wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi, kwa madai ya kupewa vibali vya
msamaha wa kodi kutoka kwa viongozi wa juu serikalini. "Mtu asije hapa
aseme amepewa kibali na Rais John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan au Waziri Mkuu, cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata
taratibu.
Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa
mujibu wa sheria," aliagiza. Waziri Mkuu alilazimika kufanya ziara hiyo
ya ghafla jana baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara huyo aliyetaka
kuudanganya uongozi wa TPA, kutaka kutoa matrela hayo yaliyoingizwa
nchini mwaka 2015 kutoka Uturuki. Bahman alitaka kupata msamaha wa kodi
kwa kuidanganya TPA, kuwa amewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza
jambo hilo, watapata matatizo.
Majaliwa alisema serikali inasisitiza watu kufuata sheria na taratibu
za nchi, ikiwemo kulipa kodi ipasavyo na inataka watendaji wake wafanye
kazi bila ya kubughudhiwa, hivyo aliwataka wafanyabiashara kufuata
sheria za nchi na kwamba serikali haina ugomvi nao.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa
matrela hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kwenye kampuni
Serin ya Uturuki. "Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa
makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania
na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka, ambayo inaonesha jina la
mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani (bill of lading) inasaidia mteja
kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakini huyu bwana
hajafanya hivyo," alisema.
Alieleza kuwa kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na
nyaraka hizo, ni kinyume cha sheria; na pia kinaweza kusababisha kampuni
iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki. Alisema
jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhoofisha uhusiano mzuri
uliopo kati ya Tanzania na Uturuki, kwani tayari kampuni hiyo
imeshawasilisha malalamiko hayo katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki
nchini.
"Uturuki wanawaamini sana wafanyabiashara wa Tanzania, sasa huu
ujanjaunja uliotumika katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na
kuyasajili magari haya bila ya kuwa na bill of lading halisi, unajenga
sura mbaya kwa wafanyabiashara wengine waaminifu na watiifu wa sheria,
nawaagiza TRA kuchukua hatua kwa wahusika, hatuwezi kupoteza mahusiano
na nchi kwa sababu ya utapeli wa mfanyabiashara mmoja," alisema.
Pia Waziri Mkuu alitoa mwito kwa mawakala wa forodha, kuhakikisha
wanakuwa makini katika kazi zao na serikali haitawavumilia wababaishaji,
kwani inasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na
si vinginevyo. Awali, Mkurugenzi wa Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit
Kakoko alimweleza Waziri Mkuu kuwa pamoja na vitisho vya mfanyabiashara
huyo kuwa wasipotekeleza matakwa yake watapata matatizo, lakini
waliendelea kusimamia sheria na taratibu.
No comments