Heade

BADO BANDARINI KUNA MAMBO


















WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema kuna uwezekano mkubwa magogo 938 yaliyopo Bandari ya Dar es Salaam na mengine yaliyomo kwenye makontena 55 bandarini hapo, hayajatoka nchini Zambia kama inavyodaiwa, bali ni maliasili ya Tanzania.

Kigwangalla alifanya ziara ya kushitukiza bandarini hapo juzi jioni baada ya kupata taarifa kuwa kuna shehena hiyo ya magogo, ambayo umiliki wake bado una utata. Alisema magogo hayo 938 yamekuwepo bandarini hapo kwa miaka 10 na mengine yaliyomo kwenye makontena 55 yapo hapo kwa miaka miwili.

Alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusu ni wapi hasa magogo hayo yametoka na yalikuwa yakisafirishwa kwenda nchi gani, Kigwangalla alisema kwa mujibu wa taarifa za kiitelejensia alizonazo ni kwamba magogo hayo mara nyingi huvunwa mkoani Rukwa na kisha kupitishiwa nchini Zambia, halafu huingizwa tena hapa nchini.

Kutokana na utata uliopo wa magogo hayo, Waziri huyo wa Maliasili ametoa siku 30 kwa wamiliki wa makontena 55 kujitokeza, wakiwa na nyaraka zote ili kuthibitisha kama kweli magogo hayo yalivunwa nchini Zambia. Alisema wakishindwa kujitokeza na kuthibitisha hilo ndani ya muda waliopewa, magogo yote yatataifishwa na kuwa mali ya Serikali.

“Nimemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yangu (Meja Jenerali Gaudence Milanzi) atangaze ili wamiliki wa magogo 938 yaliyopo bandarini kwa miaka 10 sasa, wajitokeze na wawe na nyaraka zote zinazotakiwa, wakishindwa kufanya hivyo yatakuwa mali ya Serikali,” alieleza Kigwangalla.

Kwa mujibu wa Kigwangalla na kwa mujibu wa taarifa alizonazo, magogo hayo huvunwa mkoani Rukwa na kisha huingizwa nchini Zambia kwa njia za panya. Alisema watu hao wakiwa nchini Zambia, husema kuwa magogo hayo wameyavuna Tanzania na wakiwa Tanzania wanasema wameyavuna Zambia.

Kutokana na sintofahamu hiyo, ndiyo maana ameagiza wamiliki wajitokeze wakiwa na nyaraka zinazoonesha kama kweli magogo hayo yalivunwa nchini Zambia na uhalali wa umiliki wao. Thamani ya magogo hayo haijulikana na haijajulikana ni nchi gani hasa yalikuwa yanapelekwa.

Waziri alisema analifanyia kazi hilo na thamani yake itajulikana hapo baadaye. Kigwangalla pia alilieleza gazeti hili kuwa kama wamiliki hao watashindwa kutekeleza agizo la Serikali la kujitokeza wakiwa na nyaraka hizo, mbali na kuyataifisha magogo hayo, pia wahusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali kinyume cha sheria.

Alisema magogo hayo hutumika kwa kutengeneza vitu mbalimbali kama vile samani, dawa na marashi. Alisema nchi kama ya China, hakuna kitu kinachotupwa kutoka kwenye gogo, bali kila kitu kina faida kwa kutengenezwa bidhaa fulani.

Hili ni tukio la tatu kutokea ndani ya wiki moja kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Mapema wiki iliyopita Rais John Magufuli aligundua kuwepo kwa magari madogo 50 ya kubeba wagonjwa, yaliyokwama bandarini hapo tangu Juni mwaka 2015, magari ya Jeshi la Polisi 53 yaliyokwama hapo tangu Juni 2016 pamoja na magari mengine yaliyotelekezwa bandarini hapo kwa zaidi ya miaka kumi.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alibaini mpango wa kutaka kuyaondoa bandarini hapo matrela 44 ya malori makubwa bila kulipiwa kodi huku wahusika wakilitumia jina lake.

























No comments

Powered by Blogger.