MWENDESHA bodaboda maarufu mpaka wa Sirari na Isebania, Kenya,
Kiongera Nchagwa (27) mkazi wa Kijiji cha Gwitiryo, Tarime, Mara
anasakwa na Polisi wa pande zote mbili, akituhumiwa kumuua mwenzake,
Jeremia Omera (22) kwa kumchoma kwa kisu kifuani.
Mwenyekiti wa Haki za Binadamu Wilaya ya Kurya West ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Isebania, Peter Masaithe alieleza tukio
hilo linatokana na ugomvi wa kunyang’anyana mizigo ya abiria aliyetaka
kuvuka mpaka kuingia nchini akitokea Nairobi.
“Tukio hilo la mwendesha bodaboda Kiongera Mosaisi ambaye ni
Mtanzania la kumchoma kisu kifuani mwenzake, Jeremia Omera Mgusuhi
lilitokea Jumamosi asubuhi saa 1 katika stendi ya mabasi ya Nairobi,
Isebania lililokuwa na abiria kutoka Tanzania,” alisema.
“Walianza kunyang’anyana mzigo wa abiria aliyeshuka basi la The
Guardian akivuka kwenda Tanzania. Kila mmoja alidaka huo mzigo hivyo
ugomvi ukatokea ambapo Kiongera alijihami kwa kisu na kumchoma kifuani
Jeremia na akatokwa damu nyingi hali iliyopelekea kifo chake na Kiongera
akatoroka kwa kutumia pikipiki yake na kuingia Tanzania,” alisema.
Masaithe alikemea bodaboda kutembea na visu, kunywa pombe za viroba
ambavyo baada ya kupigwa marufuku sasa vimehamia Isebania hali
inayochangia uhalifu na kuziomba serikali za nchi hizo mbili kuchukua
hatua kali ukiwemo msako wa viroba na bangi ili kuokoa vijana.
Polisi wa Isebania wamethibitisha kifo cha Jeremia na wamewasiliana
na wenzao wa Sirari kumsaka mtuhumiwa kujibu tuhuma. Polisi wa Sirari
wamekiri kupokea taarifa ya mauaji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sokoni Sirari, Benson Makanya alisema
waendesha bodaboda Sirari na Isebania wamekuwa wakitembea na silaha kama
visu na kuchangia uhalifu hapo. Mama mlezi wa Jeremia, mkazi wa Sirari,
Moraha Roman alisikitishwa na kifo chake na kusema alikulia kwao.
Aliiomba Serikali imfuatilie mtuhumiwa kwa madai mara nyingi akifanya
matukio, hutorokea Mugumu, Serengeti kwa ndugu zake na kurejea baada ya
muda. Mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Ombo Migori ukisubiri ndugu
kutoka Soneka Kisii
No comments