Heade

BENKI YA CRDB YAZIDI KUIMARISHA HUDUMA KWA JAMII

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameridhishwa na kazi inayofanywa na Benki ya CRDB ikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuenea maeneo mengi nchini, kulipa gawio la serikali pamoja na kuunganishwa na ‘TTCL data center’.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Mkoani Dodoma wakati akifungua Tawi jipya la Benki ya CRDB katika jengo la LAPF. Amesema sekta ya Benki ni Muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote hasa uchangiaji katika pato la Taifa.

Vilevile Rais amesema sekta ya Benki ni muhimu katika kupiga vita umasikini hasa katika utoaji wa mikopo kwa wananchi. Pia amesema sekta ya Benki ni muhimu sababu inasaidia katika utoaji wa Ajira za Moja kwa Moja.

Kutokana na ukweli huo Rais Magufuli akaiomba benki iendelee kutimiza jukumu lake kwa serikali “Ni matumaini yangu benki ya CRDB mtaendelea kutoa gawio letu la kila mwaka,” amesema.

Katika miongo mitatu sekta ya benki Imezidi kuimarika hapa nchini, dhamira ni kujènga viwanda, hivyo benki hazina budi kuunga mkono jitihada hizi za serikali ili hatimaye nchi iwe na uchumi wa kati. Rais ameishauri sekta ya benki hapa nchini kuongeza huduma hadi vijijini ili ziwafikie watanzania wengi zaidi.

“Natoa wito kwa mabenki nchini kusambaza huduma za kibenki hadi vijijini kwa kubuni njia za kufanya hivyo ili kuongeza ukwasi katika benki zenu” anesema Rais. “Benki Kuu ikamilishe sera ya riba ili taasisi za kifedha ziwe na riba zinazolingana, BOT msimamie kikamikifu suala la matumizi ya dola hapa nchini,” amesisitiza Rais Magufuli.

Kutokana na kukamatwa kwa dola za Marekani Bilioni Moja katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere leo, Rais akatoa neno “Zaidi ya Dola Bil. 1 zimeshikwa airport na haijulikani zilikuwa zinaenda wapi, kila benki inayokuja kufunguliwa hapa mhakikishe mnaikagua vya kutosha hasa ziwe na lengo kuwasaidia wananchi,” Amesema Rais.

Ameongeza kuwa “BOT mtusaidie benki ambazo hazifanyi vizuri na zimeshindwa kujiendesha mzifunge, na makampuni ya simu yatakayoshindwa kujiunga na mfumo wa data centre yafungwe,” amesema.

Katika hali ya kushangaza ambayo inamuonesha Rais kuwa na huruma na watanzania, Benki ya CRDB ilimpa zawadi ya shilingi milioni 100, lakini akasema badala ya kupewa yeye zipelekwe zikajenge wodi katika hospitali ya General, itakayoitwa Wodi ya CRDB.

Hundi hiyo alimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Binilith Mahenge. Baada ya kuipokea hundi hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma akasema “Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma nakushukuru Rais Dk Magufuli kwa kuamua kuhamishia Makao makuu ya nchi hapa na matokeo yameanza kuonekana,” amesema Mahenge.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei alisema ufunguzi wa Tawi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Agizo la Rais Magufuli la kuhamishia Serikali Mkoani Dodoma. “Tunakupongeza kwa mengi uliyoyafanya katika kipindi kifupi cha uongozi wako, ambayo yameonesha tija kwa taifa.

Tumeanza kuona mwanga kwenye nchi yetu ya kufufua uchumi wa nchi. Tunaipongeza Serikali yako kwa uamuzi wa ukusanyaji wa Kodi kwa kutumia mifumo ya kielektroniki,” amesema Dk Kimei.

Mpaka sasa Waziri Mkuu, Mawaziri, Makatibu wakuu wameshahamia Dodoma, na katikati ya mwezi Disemba Makamu wa Rais atahamia hapa na ambapo mwakaniRais naye atakamilisha zoezi la kuhamia Dodoma.

No comments

Powered by Blogger.