YOHANA Chengula (71) na Aloyce Mwalongo (80) ni miongoni mwa wafungwa
61 ambao kamwe hawataisahau Desemba 9, 2017, siku ambayo waliachiwa
huru kutoka gerezani.
Wafungwa hao walipata msamaha wa Rais John Magufuli wakiwa wamesota
gerezani kwa takribani miaka 44. Walikuwa wakitumikia adhabu
iliyobadilika kutoka kunyongwa na kuwa kifungo cha maisha baada ya
kutiwa hatiani kwa makosa ya mauaji mwezi Machi mwaka 1978.
Rais Magufuli alitoa msamaha huo wakati wa maadhimisho ya Miaka 56 ya
Uhuru ambapo wafungwa 8,157 waliokuwa wamehukumiwa kwa makosa
mbalimbali walinufaika na msamaha huo.
Chengula akuta mke watoto 4 wamefariki dunia Akizungumzia maisha
mapya nje ya gereza, Chengula alisema: “Nashukuru kwa sasa nipo uraiani
nimepata fursa ya kuona ndugu zangu waliobaki, wajukuu na mwanangu pekee
aliyebakia baada ya wale wanne niliozaa na mke wangu wa kwanza
kufariki, sasa nafsi yangu ipo huru nikiamini hata kama Mungu
ananichukua nitakuwa kwenye mikono yao.
“Mke wangu aliyesababisha mimi nikapatwa na masahibu haya naye
niliambiwa alishafariki dunia, sina kinyongo naye na nina muombea amani
huko alipotangulia nikiamini sisi binadamu sote njia yetu ni moja, si
ajabu hata kesho mimi au wewe tunaweza tukaitwa na Mwenyezi Mungu
aliyetuumba,” alisema Chengula.
Alisema mbali na msamaha mkubwa alioupata kutoka kwa Rais Magufuli,
anamuomba asiache kumuangalia yeye na wafungwa wenzake walioachiwa
ikibidi kuwawezesha kwa chochote kutokana na hali mbaya ya kiuchumi
waliyonayo na mazingira ya huko kijijini wanayokwenda kuishi mara baada
ya kuwa huru.
“Tunarudi kijijini, hatuna ndugu wala familia tena…tunakwenda kuanza
maisha upya nasi ni wazee, hatuna jipya la kufanya huko tuendako zaidi
ya kupambana na hali ya umasikini nami ndiyo kama unavyoniona niliingia
gerezani nikiwa mzima na sasa nikiwa mlemavu.”
Aidha Chengula amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
kumsaidia mguu utakaomwezesha kutembea akidai kuwa alipata taarifa
kuhusu uwezeshaji wa viungo bandia unaofanywa na Makonda akiwa gerezani,
huku naye akiwa mmoja wa walemavu walioandika barua kuomba kusaidiwa.
Mwalongo naye akuta majonzi nyumbani Kwa upande wake Mwalongo ambaye
mwili wake bado unaonekana upo imara licha ya uzee alionao, alisema
aliingia gerezani kutokana na kesi hiyo akiwa kijana wa miaka 35 huku
akiacha mke na watoto watano wa kuwazaa na mkewe ambaye kwa sasa ni
marehemu. “Ukiacha mke wangu, pia watoto wangu watatu nao wamefariki
dunia.
Utaona ni matatizo kiasi gani yameipata familia yangu… ila naamini
hii yote ni mipango ya Mungu kwa kuwa yameshatokea basi, ila tunashukuru
Mungu tunarudi nyumbani japo tuweze kuhani katika makaburi yao.”
Alisema alikwenda gerezani akiamini mwisho wa maisha yake yote yatakuwa
humo, lakini Desemba 9, mwaka huu imebadilisha kile alichokiamini miaka
yote baada ya kupewa msamaha na Rais Magufuli.
Alisema tangu waingie gerezani ni awamu tatu za marais zimepita,
hivyo kitendo cha Rais Magufuli kutoa msamaha kwao, kinaonesha wazi ni
namna gani Mungu anaweza kutenda miujiza…zaidi anamshukuru kwa moyo wake
wa huruma aliouonesha kwao na kwa wafungwa wengine waliopata msamaha
huo. Aidha alisema kwa kuwa sasa wanarejea kijijini mkoani Njombe,
hawana namna nyingine ya kuendesha maisha yao zaidi ya kuwa tegemezi
kutokana na hali waliyonao baada ya kutoka gerezani.
“Ningependa kuwa mfugaji kama nikibahatika kupata mifugo, sina jambo
lolote la msingi nitakalokwenda kulifanya kwa sasa zaidi ya kukaa
nyumbani na kulea wajukuu hivyo nikipata msaada wa kuwezeshwa japo
mifugo nitashukuru.”
Chengula na Mwalongo ni kati ya wafungwa watano waliohukumiwa adhabu
ya kunyongwa, lakini walibadilishiwa adhabu hiyo na kuwa kifungo cha
maisha katika msamaha uliotolewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Kwanza,
Mwalimu Julius Nyerere, Aprili 18, 1983. Chengula na kisa cha kukatwa
mguu Akizungumzia mkasa mzima Chengula ambaye kwa sasa ni mlemavu akiwa
na mguu mmoja, anasema: “Chanzo cha matatizo haya yote ni mke wangu
niliyezaa naye watoto wanne ambaye hadi matatizo yananipata nilikuwa
nimeshatengana naye.
“Vitendo vyake vya uhuni ndivyo vilivyosababisha mimi na wenzangu
kupewa kesi ya mauaji ya raia mmoja wa India, wakati huo wote tukiishi
mjini Njombe mkoani Iringa. “Nakumbuka siku ya tukio, wakati huo nikiwa
na miaka 28, mimi na marafiki zangu tulikuwa nyumbani tukiendelea na
maongezi huku tukipata soda na bia, vinywaji nilivyokuwa nikiiuza katika
baa yangu, tukiwa hatuna hili wala lile ghafla tulisikia kelele za moto
kutoka nyumba ya jirani umbali mfupi kutoka kwangu, ndipo ikatulazimu
sote tutoke kwa ajili ya kwenda kutoa msaada”.
Alisema baada ya kufika walikosa namna ya kuokoa chochote kutoka
ndani ya nyumba hiyo kutokana na moto mkali uliokuwa ukiwaka, lakini
baada ya muda mfupi walipata usaidizi kutoka kwa wanajeshi waliokuwa
wakipita kuelekea Songea ambao waliisogelea nyumba hiyo na kupiga mlango
teke kuona kama kuna mtu yeyote angeweza kutoka ingawa hawakuwa na
uhakika kama kulikuwa na mtu.
Alisema baada ya muda kidogo polisi walifika wakati huo moto ukiwa
umezima na waliingia ndani ya nyumba hiyo na kutoka na mwili wa raia
huyo wa India akiwa ameshafariki dunia baada ya kuteketea kwa moto.
“Baada ya tukio hilo tulikaa mtaani kwa siku kadhaa huku nikiendela
na biashara zangu ikiwemo ya usafirishaji abiria na mizigo nikitumia
gari yangu mwenyewe aina ya Toyota Stout niliyoinunua kwa Sh 15,000
kipindi hicho, lakini ghafla Oktoba 30, 1974 jioni, nilishitukia
nafuatwa na polisi wakinitaka kwenda kuhojiwa kutokana na kifo cha mtu
huyo.
“Sikuwa na wasiwasi pale nilipofuatwa kwa kuwa nilijua wazi kuwa
sikuhusika na kitu chochote kutokana na kifo cha mtu huyo ambaye kwa
kipindi fulani pia aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa
mke wangu ambaye kwa kipindi hicho nilikuwa tayari nimeshamuacha.
“Ndiyo maana hadi sasa nasema aliyekuwa mke wangu ndiyo hasa chanzo
cha mimi na wenzangu kwenda jela kwa sababu kama angekuwa ametulia ndani
ya ndoa tusingekuwa tumeachana naye na baadaye yeye kuwa na uhusiano na
mtu huyo ambaye kifo chake kilihusishwa na fikra kuwa mimi nilihusika
kutokana na uhusiano wake na mke wangu.”
Alisema alipofika polisi aliwakuta marafiki zake wanne wakiendelea
kuhojiwa na baada ya hapo walipelekwa Gereza la Iringa wakisubiri kesi
yao kusomwa wakati huo ikiwa tayari wameshakaa jela kwa takribani miaka
minne.. ..na ilipofika Machi 14, 1978 ilitolewa hukumu ambayo ilibadili
ndoto zao zote za kimaisha. Alisema katika hukumu hiyo yeye na mwenzie
mmoja aliyekuwa akitekeleza kifungo chake katika Gereza la Isanga Dodoma
walihukumiwa kunyongwa, wengine wawili waliwekwa gerezani wakisubiri
kutolewa kwa amri ya Rais huku mmoja wa mwisho (Mwalongo) akipewa adhabu
ya kifungo cha miaka 10 gerezani.
“Hukumu yenyewe ilimshangaza kila mmoja, lakini tunaamini kuwa yote
haya yalipangwa kwetu kwa sababu maalumu, kwani hata mazingira ya kesi
yenyewe na ushahidi ulijawa na uongo mtupu, pia mazingira ya kesi
yenyewe yalikuwa na utata yaani kimsingi ni jambo tulilokuwa
tumeandaliwa lituhusu,” alisema Chengula.
Mateso gerezani Chengula alisema kilichomuuma wakati akiwa gerezani
ni familia yake, na hasa mke wake mdogo ambaye wakati anapewa hukumu
hiyo alimuacha akiwa na mtoto mwenye umri wa wiki mbili (Feines
Chengula), ambaye kwa sasa ni mwalimu mkoani Morogoro alipoamua
kuikimbia familia yake na kuiacha ikitangatanga.
“Mbali na mke wangu na mtoto wangu huyo mdogo niliyezaa naye, lakini
pia niliacha watoto wanne niliokuwa nimezaa na mwanamke niliyeachana
naye, ambao aliwatelekeza. “Lakini pigo lingine ilikuwa ni biashara
zangu za maduka, nyumba ya kulala wageni pamoja na gari yangu ambavyo
vyote vilitaifishwa na Polisi kwa madai kuwa nyumba yangu ilihusika
katika kuhamisha mali zilizokuwa kwenye nyumba ya mhindi huyo kabla ya
kuteketea.”
Chanzo cha kukatwa mguu Alisema akiwa gerezani, maisha yake
yalikumbwa na misukosuko ya kila aina lakini kubwa ni magonjwa yakiwemo
kipindupindu kilichompata akiwa Gereza la Isanga Dodoma, na kisukari
kilichompata akiwa gerezani mkoani Morogoro ambacho baadaye mwaka 2003
kilifanya ahamishiwe katika Gereza Kuu la Ukonga.
Chengula alisema akiwa Gereza la Ukonga hali yake ilianza kuwa mbaya
na kusababisha mguu kujaa maji kutokana na ugonjwa wa kisukari, hatua
ambayo baadaye ililazimu kukatwa kwa mguu huo katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili ili kumuokoa dhidi ya kifo alichodai kuwa kwa wakati huo
aliona dalili za waziwazi kuwa kilikuwa kinamuita.
Alisema akiwa katika Gereza la Ukonga aliendelea kumuomba Mungu usiku
na mchana huku akiamini kabisa siku zake za kuishi gerezani huko
zikienda ukiongoni kutokana na uzee aliokuwa nao ukichanganya na maradhi
ya hapa na pale yaliyokuwa yakimkabiri. Shemeji atoa ushuhuda Kwa
upande wake Rosemary Mkwama ambaye ni shemeji wa Chengula, alisema
wakati shemeji yake huyo akikamatwa alikuwa na umri mdogo na wakati huo
alikuwa akisubiri matokeo yake ya mtihani wa darasa la saba.
Alisema wakati huo alikuwa akiishi kwa Chengula ambaye mdogo wake
alikuwa mume wa dada yake huku yeye akilelewa katika ukoo huo, wakiishi
kwa amani mustarehe pasina shaka yoyote hadi siku walipofika polisi
katika nyumba wanayokaa na kumkamata shemeji yake.
Alisema wanashukuru kwa kuwa sasa ndugu yao huyo yupo uraiani, huku
wakitoa pongezi na shukrani kwa Rais Magufuli kwa kitendo chake cha
kuwaachia huru wakiamini kuwa walionewa. Alisema wanatarajia Chengula
ataanza safari ya kuelekea Njombe leo huku baadhi ya ndugu zake kutoka
maeneo mbalimbali nchini na wanakijiji aliokuwa akiishi nao wakimsubiri
kwa hamu ili waweze kumsabahi na kumkaribisha kuanza upya maisha ya
uraiani kijijini Njombe.
No comments