WITO umetolewa kwa wafanyabiashara kutoka nchi za Kenya, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia, Malawi na Uganda kujitokeza kununua
dagaa waliofurika katika Soko la Samaki Kirumba Mwaloni, jijini Mwanza.
Ziwa Victoria lipo katika nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda,
lakini Tanzania ikiwa na eneo kubwa la ziwa hilo, asilimia 49. Kenya ina
asilimia sita na Uganda ina asilimia 45.
“Kwa sasa dagaa na samaki wengine wanapatikana kwa wingi sokoni hapa,
hivyo tunawakaribisha wateja wetu wakuu kutoka Kenya, DRC, Zambia,
Malawi na hata Uganda kuja kununua bidhaa hizi.
“Wateja wetu wengine wakuu ni kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini
ikiwamo Dar es Salaam, Mtwara na Pwani, hao wote tunawakaribisha, dagaa
wapo wa kutosha,” alisema Mwenyekiti wa soko hilo, Fikiri Magafu katika
mahojiano na gazeti hili jijini hapa, jana.
Kwa mujibu wa Magafu, dagaa na samaki wengine wakiwamo aina ya
sangara wanaovuliwa katika Ziwa Victoria wameongezeka sokoni hapo tangu
Novemba mwaka huu kutokana na ongezeko la maji ziwani kipindi hiki cha
mvua zinazoendelea kunyesha.
Hata hivyo, alielezea kuridhishwa na mahudhurio ya wafanyabiashara
kutoka DRC akisema wamejitokeza saba katika kipindi cha wiki mbili na
kwamba kila mmoja ameweza kununua magunia kati ya 100 na 1,000 yenye
dagaa.
Naye muuzaji wa dagaa katika soko hilo, Johari Juma alitoa wito kwa
serikali ya Tanzania kulitangaza soko hilo kimataifa na kupunguza ushuru
wa bidhaa hizo ili kuvutia zaidi wanunuzi kutoka nje ya nchi.
Soko la Samaki Kirumba Mwaloni lina uwezo wa kuhifadhi magunia 80,000
yenye dagaa kwa wakati mmoja, achilia mbali samaki wengine, matunda na
nafaka mbalimbali. Soko hilo lipo kando ya Ziwa Victoria na lina uwezo
wa kuhudumia jumuiya ya wafanyabiashara zaidi ya 2,000 wa samaki kwa
wakati mmoja.
No comments