Hali ya upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na vyoo katika vituo
vya huduma za afya maeneo ya vijijini bado ni changamoto, huku asilimia
44 pekee ndio vina huduma hiyo.
Kati ya hizo, asilimia 34 ya vituo hivyo vimebainika kuwa bado vinatumia
maji kutoka katika vyanzo ambavyo si salama, ambavyo ni mito, maziwa,
visima visivyofunikwa na mabwawa, huku asilimia 56 zikikosa kabisa uwapo
wa huduma hizo muhimu.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti wa tathmini ya upatikanaji wa
huduma muhimu katika vituo vya afya wa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wengine.
Ili kukabiliana na hali hiyo, jana Serikali imezindua Mwongozo wa Taifa
wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya.
Mwongozo huo umezinduliwa na Mkurugenzi wa Uratibu wa Kisekta wa Ofisi
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Andrew Komba kwa niaba
ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubsya.
Akizungumza kuhusu mwongozo huo, Mratibu wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa
Mazingira, Anyitike Mwakitalima alisema umeandaliwa kuboresha utoaji
huduma katika vituo vya afya nchini.
“Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi kwa muda mrefu kutokana
na kutokuwapo kwa mwongozo wa Taifa ambao utasaidia kusimamia ubora wa
utoaji huduma katika vituo vya afya ikiwamo ujenzi wa vyoo bora na
upatikanaji wa maji safi.
“Tulibaini pia asilimia 42 ya vituo havina sehemu maalumu za kunawia kwa
ajili ya watoa huduma za afya kunawa mikono katika vyumba vya
kujifungulia, hali hii ni mbaya ikiwa hatutachukua hatua, kuna uwezekano
wa watoto wanaozaliwa kupata athari mbalimbal,” alisema.
Awali, Dk Komba alisema mwongozo huo utasaidia Serikali na wadau wa
maendeleo kusimamia na kutekeleza masuala ya usafi wa mazingira.
“Mwongozo unatoa maelekezo stahiki namna ambavyo vituo vya afya katika
ngazi zote vinavyopaswa kufanya katika upangaji mipango na uandaaji wa
bajeti zitakazotumika katika usimamizi wa usafi wa mazingira,” alisema.
Mkurugenzi wa Mipango wa Shirika la WaterAid, Abel Deganga alisema
kutokana na kukosekana kwa mwongozo kwa muda mrefu unaopima hali ya
upatikanaji maji katika vituo vya afya nchini, utendaji kazi wa Serikali
na wadau ulikuwa ukisuasua.
No comments