Heade

RAIS JOHN MAGUFULI AKUTANA NA MWEKEZAJI BOMBA LA HOIMA

RAIS John Magufuli amekutana na viongozi wa kampuni ya Total ambayo ni mwekezaji mkubwa wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga.

Katika kikao hicho Rais Magufuli amewahakikishia viongozi hao kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kwa kampuni hiyo na washirika wengine katika ujenzi wa mradi huo. Viongozi wa Total waliokutana na Rais Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam jana ni Rais wa Masoko na Huduma, Momar Nguer, Rais wa Total Africa, Stanislas Mittelman, Makamu wa Rais wa Total wa Afrika ya Kati na Afrika Mashariki, Jean Christian Bergeron na Mkurugenzi Mtendaji Total Tanzania, Tarik Moufaddal.

Rais Magufuli aliitaka Total kuharakisha ujenzi wa bomba hilo uliopangwa kuanza mwezi ujao na kukamilisha mapema hata kabla ya mwaka 2020 ili wananchi wa Tanzania na Uganda waanze kunufaika na mafuta hayo.

“Tuna matumaini makubwa na Total kuwa kazi hii mtaifanya haraka, na naomba niwahakikishie kuwa pamoja na soko la nje, kuna soko kubwa Afrika Mashariki lenye watu milioni 165, na Serikali ya Tanzania itawapa ushirikiano wa kutosha wakati wote wa ujenzi na uendeshaji wa mradi ili mradi mnalipa kodi vizuri na mnazingatia sheria zetu,” alisisitiza Rais Magufuli.

Aliitaka kampuni hiyo kuzingatia kutoa ajira kwa Watanzania katika wilaya 24 ambazo bomba litapita huku akiwahakikishia kuwa Tanzania inao wakandarasi na wahandisi wa kutosha na wenye uwezo wa kushirikiana nao katika ujenzi wa bomba hilo.

Baada ya mazungumzo hayo, Waziri wa Nishati Medard Kalemani na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage walisema pamoja na kuja nchini kuangalia maandalizi ya ujenzi wa bomba, viongozi wa Total wameamua kuimarisha soko la mafuta Tanzania na pia kushirikiana na Serikali katika utafiti wa mafuta katika maeneo ya Ziwa Tanganyika, Eyasi Wembere na Ziwa Rukwa.

Kwa upande wake Momar Nguer alimshukuru Rais Magufuli na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kwa msukumo mkubwa walioutoa katika kufanikisha mradi huo na aliahidi kuwa Total itahakikisha inakamilisha haraka mambo machache yaliyobaki ili kuanza ujenzi bila kuchelewa.

No comments

Powered by Blogger.