Wataalamu wa jiolojia wamesema kuwa tetemeko la ardhi limetokea Kata ya
Aneti wilayani Chamwino usiku wa kuamkia jana lina ukubwa wa 5 katika
kipimo cha richter.
Tetemeko lenye ukubwa wa 5.1 kipimo cha richter lilitokea Julai mwaka
juzi katika kata hiyo na kusababisha nyumba zaidi ya 60 kupata nyufa.
Ofisa Mwandamizi wa Jiolojia katika Wakala wa Jiolojia Nchini (GST),
Gabriel Mbogoni alisema tetemeko hilo limetokea katika maeneo
lilipotokea mwaka jana Kusini
Mashariki wa mji wa Aneti.
Alipoulizwa kama tetemeko hilo lililotokea saa 9 limeleta madhara yoyote, Mbogoni alisema hajapata taarifa.
“Ukubwa wa 5 siyo la kawaida. Unakumbuka la Bukoba lilikuwa na ukubwa
gani? Ni kama 5.7 tetemeko linaweza likawa na ukubwa wa tano hadi saba
lakini lisilete madhara,” alisema.
Mbogoni alisema tetemeko linaweza likawa na ukubwa mdogo lakini likaleta
madhara kutegemea na mpasuko wa miamba umetokea katika kina gani.
“Inategemea pia na eneo ambalo mawimbi yanapita, ile miamba iko namna gani,” alisema Mbogoni.
Alifafanua kuwa tetemeko hilo lilipiga kati ya sekunde nne na tano na
kwamba likipiga kati ya sekunde 20 hadi 30 madhara yake ni makubwa sana.
Mbogoni alisema madhara hayo yanatokana na jengo kutikiswa kwa muda ambazo tetemeko linadumu.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga alisema hadi jana mchana kulikuwa hakujaripotiwa madhara yoyote.
“Nimewasiliana na viongozi wa kule, diwani na mwenyekiti wa kitongoji
wanasema ni kweli lilitokea lakini hadi sasa hakujaripotiwa madhara
yoyote,” alisema.
Tetemeko kubwa la ardhi kutokea nchini lilitokea miaka tisa iliyopita
katika eneo la Oldonyo Lengai ambalo lilikuwa na ukubwa wa 5.9 kwa
kipimo cha richter.
No comments