Heade

MAHAKAMA YA KENYA HAINA TAARIFA YA KUAPISHWA KWA ODINGA

Nairobi, Kenya. Mahakama imesema haijapata mawasiliano rasmi kutoka kwa Muungano wa Nasa kuhusu hatua ya kumuapisha kiongozi wake Raila Odinga.

Msajili Mkuu wa Mahakama, Anne Amadi amesema Mahakama haina taarifa kuhusu sherehe iliyopangwa kufanyika Desemba 12,2017.

“Hatujaarifiwa chochote kuhusu hafla ya kumuapisha Raila Odinga inayopangwa na muungano wa upinzani,” amesema.

Muungano wa Nasa umeanza matayarisho ya hafla ya kumuapisha kiongozi huyo kwa kuunda kamati ya kusimamia shughuli hiyo.

Kuteuliwa kwa kamati hiyo ya watu saba kumefanyika siku chache baada ya Odinga kutangaza Jumanne iliyopita kuwa ataapishwa kupitia mabunge ya kaunti, hatua ambayo Serikali imesema ni kinyume cha sheria.

Gazeti moja la Kenya limesema muungano huo umetuma kadi za mwaliko wa hafla hiyo iliyopangiwa kufanyika Desemba 12,2017 Taifa hilo litakaposherehekea siku ya uhuru.

Kadi za kidigitali za mwaliko zenye jina la Odinga hazionyeshi mahali hafla hiyo itafanyika.

“Umekaribishwa. Njoo ushuhudie rais wa wananchi Raila Amollo Odinga akiapishwa tarehe 12 Desemba saa sita mchana. Taarifa kuhusu itakapoandaliwa hafla hii itatolewa baadaye,” ndivyo inavyosomeka kadi hiyo ambayo inasisitiza kuwa inaruhusu mtu mmoja pekee kwa kila kadi.

Kamati hiyo ambayo itakuwa ya kitaifa ya kuendesha mabunge ya wananchi, itaongozwa na msomi wa uchumi maarufu, David Ndii.

No comments

Powered by Blogger.