Marekani
imesema iko tayari kwa mazungumzo na Korea Kaskazini "bila masharti",
ingawa inaendelea kutathmini njia zote, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa
kutumia nguvu za kijeshi, ili Pyongyang iachane na mpango wake wa silaha
za nyuklia.
Wakati huo huo
ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, alikuwa akitoa
tangazo hilo ambalo linaonyesha jinsi gani Marekani imeanza kulegeza
msimamo wake, Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un ameendelea
kuongeza vita vya maneno katika miezi ya hivi karibuni, akionyesha nia
yake ya kuifanya nchi yake kuwa yenye "nguvu kubwa za nyuklia na kijeshi
duniani".
Hata hivyo hali hiyo haikatazi Pyongyang "kukubali kuwa
ni muhimu kuepuka vita na Marekani," amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa wa Mambo ya Kisiasa, Jeffrey Feltman, ambaye ni raia wa
Marekani.
Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa alielezea siku
ya Jumanne katika kikao cha faragha cha Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa ziara yake wiki iliyopita nchini Korea ya Kaskazini, ambapo
Pyongyang ilishutumu Marekani kutaka kuanzisha vita na Korea Kaskazini".
Mpaka
sasa, utawala wa Donald Trump umekua ukisema kuwa uwezekano wa
mazungumzo na Korea ya Kaskazini hayawezi kufanyika kwa muda mrefu kwa
sharti ya kupokonywa silaha za nyuklia.
"Sio sahihi kusema"
tutazungumza nanyi ikiwa mtakuja kwenye meza ya mazungumzo mkiwa tayari
kuacha mpango wenu wa nyuklia, "alisema Tillerson siku ya Jumanne katika
mkutano mjini Washington. "Wamewekeza kiasi kikubwa katika sekta hiyo,"
Bw Tillerson alisema kuhusu suala la maendeleo ya makombora ya masafa
marefu yanayokwenda hadi bara jingine na silaha za nyuklia
vinavyotengenezwa na Korea Kaskazini.
"Tuko tayari kuzungumza kwa
wakati wowote Korea ya Kaskazini itakua tayari kuzungumza," alisema.
"Tuko tayari kufanya mkutano wa kwanza bila masharti".
No comments