Haider Gulamali ambaye ni mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia mjini
Dodoma, ameibuka wa kwanza kwenye kura za maoni kugombea nafasi ya
ubunge kwa tiketi ya CCM jimbo la Singida Kaskazini kwa kupata asilimia
60.
Gulamali aliwabwaga vibaya wagombea wengine 21 wa kinyang'anyiro
hicho huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Elia Digha
aliyedaiwa kuwa tishio akishindwa kurejesha fomu yake kwa muda
uliopangwa, hivyo kujiondoa mwenyewe kwenye mpambano.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu Mwenezi
wa CCM mkoa wa Singida, Hamad Athumani, Gulamali alijikusanyia kura 606
kati ya kura halali 1,009 zilizopigwa.
Justine Monko ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji katika Halmashauri ya
Liwale mkoani Lindi alichukua nafasi ya pili baada ya kujipatia kura 133
huku aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Huduma za Misitu Nchini, Juma Mgoo
akiambulia kura 46 na Sabasaba Manase kura 39.
Katika mchakato huo wa kura za maoni, Aaron Mbogho ambaye ni Mkuu wa
wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro aliambulia kura tatu tu. Jimbo la
Singida Kaskazini limekuwa wazi tangu Oktoba mwaka huu baada ya
aliyekuwa Mbunge wake, Lazaro Nyalandu kukosa sifa kufuatia kufukuzwa
uanachama wa CCM kwa kitendo chake cha kuhamia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema).
No comments