ZAIDI ya wanafunzi 100 waliohitimu kozi ya afya katika Chuo cha
Sayansi ya Afya St. Aggrey jijini Mbeya, mwaka 2017, wamekilalamikia
chuo hicho kwa kushindwa kuwarejeshea vyeti halisi vya kidato cha nne.
Vyeti hivyo ni vile walivyotakiwa kukusanywa, kwa madai ya kwenda
kuhakikiwa Wizara ya Afya. Hayo yamesemwa na Rais mstaafu wa Serikali ya
wanafunzi wa chuo hicho, Noeli Mng’ong’o. Alisema hayo alipokuwa
akizungumzia adha wanazokumbana nazo, ikiwamo kukosa fursa za ajira
serikalini na katika taasisi binafsi kutokana na ukosefu wa vyeti halisi
vya kidato cha nne.
Alisema mwaka 2015 wanafunzi 112 walijiunga na chuo hicho kwa kozi ya
afya ngazi ya jamii kwa kipindi cha mwaka mmoja. Alisema uongozi wa
chuo uliwataka wawasilishe vyeti halisi vya kidato cha nne ili vipelekwe
Wizara ya Afya kwa ajili ya uhakiki, kama ni kweli walihitimu au la.
Alisema tangu wakabidhi vyeti hivyo Novemba 2015, wamekuwa wakividai
kwa uongozi wa chuo, lakini hadi sasa wamekuwa wakizungushwa na hakuna
majibu yoyote. “Mkuu wa Chuo, Dk Rex Mwakipiti anadai wamefuatilia
wizarani wameambiwa havipo na wala haijawahi kupokea vyeti halisi kutoka
chuo hicho,” alisema Mng’ong’o.
Mkuu huyo wa chuo alipotafutwa kwa njia ya simu, kuzungumzia suala
hilo, alidai yupo kwenye kikao na kwamba atafutwe wakati mwingine.
Mng’ong’o alisema mkuu huyo aliwaeleza kuwa Wizara ya Afya, inadai
hawana hata nyaraka zinazothibitisha kama chuo hicho kiliwahi
kuwasilisha vyeti halisi vya kidato cha nne vya wanachuo hao kwa ajili
ya uhakiki.
No comments