RAIS John Magufuli amerudisha kwa wananchi ekari 129 za ardhi
zilizochukuliwa na serikali kwa ajili ya kutumika kuzikia viongozi wakuu
wa nchi.
Aidha, ametaka taasisi au mashirika ambayo yanataka kuchukua eneo
hilo, wahakikishe wanawalipa fidia wananchi waliopo na kuagiza wananchi
hao waipe thamani ardhi hiyo. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa nyumba
150 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Iyumbu, Dodoma,
Rais Magufuli alisema kuwa sheria ya kutaka kutengwa kwa eneo kwa ajili
ya kuzikia viongozi wakuu, ilipitishwa wakati akiwa Waziri.
Alisema kuwa alipanga endapo akifa akazikwe nyumbani kwao Chato na
sio Dodoma na kwamba hakutarajia kwamba angekuwa Rais. ‘’Baada ya kuwa
Rais, ndio nimeona hii sheria inapaswa kubadilishwa, kwa kuwa
nilizungumza na kiongozi mmoja kuhusu suala hili la kuzikwa hapa Dodoma
naye amekataa, hivyo nataka sheria hii ibadilishwe na wananchi
warudishiwe ardhi yao,’’ alifafanua.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Dodoma, Anthony Mavunde kuomba
ardhi hiyo, ambayo serikali iliichukua kwa lengo la kuzikia wananchi,
irudishwe kwa wananchi kwani hakuna fidia yoyote, ambayo serikali
imelipa na eneo halifanyiwi kitu chochote. Rais Magufuli alisema kuwa ni
lazima wananchi warudishiwe ardhi yao na waiendeleze, kwa kuwa thamani
yake imepanda ambapo wanaweza kufaidika nayo.
‘’Shirika linalotaka kuchukua ardhi hii wawalipe fidia wananchi
hawa…tena nawaomba msiondoke katika maeneo yenu hadi mlipwe…hata kesho
limeni, pandeni komamanga, mipapai kuipa thamani ardhi yenu,’’
alisisitiza. Pia alisema kwa kuanzia leo wananchi wowote watakaohitaji
kuuziwa ardhi, wawapatie kwa kuwauzia vipande vipande, iwe wenyeji wa
mkoa huo au hata kutoka mikoani.
‘’Mgogo akija mkatieni vipande vipande muuzieni, mkimuona Mzaramo
amekaa vibaya muuzieni ardhi hii, lakini akija Msukuma mpeni bure…ninyi
ni watani zangu, hivyo nataka mfaidike na ardhi hii,’’ alisema Rais
Magufuli.
Aidha, alisema kuwa nyumba hizo zilizojengwa kwa kiwango cha juu na
NHC, wapewe Idara ya Uhamiaji ili wafanyakazi wake waishi, zisikae bure
na kwamba serikali itaendelea kufanya hivyo kwa jeshi la polisi na
magereza. Alipongeza idara hiyo ya Uhamiaji kwa kazi nzuri wanayoifanya
kukamata wahamiaji, tofauti na miaka ya nyuma na kuwataka kuendelea
kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Aliongeza kuwa NHC iwaambie mkopo wa Sh bilioni 200 wanaotaka,
watarudisha kwa namna gani bila kuhusisha serikali. Wakati huo huo, Rais
Magufuli aliwataka wakazi wa Dodoma kutumia fursa iliyopo katika
kujiingizia mapato, ambapo tayari watumishi 3,000 wameshahamia jijini
humo. Alisema kuwa kumekuwa na mikutano mbalimbali ya chama na taasisi
inayoendelea kufanyika jijini humo, ambapo watu wengi wanatafuta mahali
pa kulala na kuamua kulala Singida wakati wangeweza kulala Dodoma.
‘’Muache majungu na kambi sijui za Malecela, mara nani, ili kuleta
maendeleo, hii ni nafasi pekee ya kutangaza mkoa na kutengeneza maisha
yenu na nimefanya makusudi kumleta Mkuu wa Mkoa huyu ili kuleta
maendeleo,’’ alisema Rais Magufuli na kuongeza; ‘’Kama leo (kesho)
kutakuwa na mkutano wa walimu wote Tanzania watahitaji vyumba vya
kulala, lakini inashangaza kuona hakuna gesti za kutosha za kulala hawa
watu. Mtumie fursa hii vizuri na viongozi wenu kufaidika kiuchumi,’’
alisema.
No comments