RAIS John Magufuli ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kudhibiti
matumizi ya fedha za kigeni katika biashara na huduma nchini ili kulinda
nguvu ya fedha ya Tanzania na kukabiliana na uhalifu wa kifedha.
Pia, ameitaka BoT kuongeza usimamizi wa benki zinazoendesha shughuli
zake hapa nchini, ikiwemo kuhakikisha zinajiunga na mfumo wa ukusanyaji
mapato kwa njia ya kielektroniki na kufuatilia kwa ukaribu utendaji wake
wa kila siku ili ziwe na manufaa kwa nchi. Alitoa maagizo hayo jana
wakati akifungua tawi la Benki ya CRDB-LAPF Dodoma na kubainisha kuwa
hatua hiyo itasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.
“Hivi sasa kuna benki 58 hapa Tanzania, BoT ni lazima mzifuatilie kwa
ukaribu benki hizi, na zile zisizofanya vizuri chukueni hatua mara
moja, ni bora tubakiwe na benki chache kuliko kuwa na benki nyingi
zinazofanya vibaya.
“Pia nataka mdhibiti matumizi ya dola, hivi navyozungumza kuna dola
milioni moja zimekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
jijini Dar es Salaam, hakuna maelezo yoyote juu ya kuingia fedha hizo,
ni lazima tuwe makini,” alisisitiza Rais Magufuli.
Aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuendeshwa kwa ufanisi tangu
ilipobinafsishwa kutoka serikalini, ambapo katika kipindi cha miaka 10
imelipa kodi serikalini kiasi cha Sh bilioni 800, imetoa ajira kwa
Watanzania 3,200, imetoa gawio serikalini la Sh. bilioni 19.5 mwaka huu
na imetoa mikopo yenye thamani ya Sh. trilioni 3.5 ambapo Sh trilioni 1
kati yake zimeelekezwa katika sekta ya viwanda na kilimo.
Kuhusu kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, Rais
Magufuli alisema serikali imechukua hatua mbalimbali zitakazoongeza kasi
hiyo, zikiwemo kupunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana za
benki za biashara, kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu kutoka asilimi 10
hadi 8. Hatua nyingine ni kushusha riba ya Benki Kuu mara mbili kutoka
asilimia 16 hadi 9, kutoa mikopo maalumu kwa benki za biashara na Benki
Kuu kununua fedha za kigeni kwenye soko la jumla la benki ili kuongeza
ukwasi wa shilingi kwenye uchumi.
No comments