RAIS John Magufuli amewahakikishia walimu wote nchini kuwa serikali
ipo tayari kulipa madeni ya walimu, baada ya madeni hayo kuhakikiwa.
Alisema hayo mjini Dodoma jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama
cha Walimu Tanzania (CWT). Pamoja na kulipa madeni ya walimu, Rais
Magufuli alisema serikali inawajali walimu na ipo tayari kuboresha
maslahi yao na kuboresha mazingira ya kazi kulingana na uwezo wake.
Aliwataka Watanzania wakiwemo walimu, kuchapa kazi kwa juhudi na
maarifa ili nchi iwe na fedha za kutosha kuongezea maslahi hayo. Hata
hivyo, alitoa mwito kwa walimu kuangalia upya matumizi ya michango ya
asilimia mbili ya mshahara, anayokatwa kila mwalimu kila mwezi kwa ajili
ya kuendesha CWT.
Alibainisha kuwa fedha zinazokusanywa ni nyingi na zingeweza kutumika
kuwasaidia walimu, badala ya kuwekezwa katika miradi ambayo haimsaidii
Mwalimu. Alitoa mfano wa mradi wa Benki ya Walimu, ambao mpaka sasa
haujaanza na kuweka wazi kuwa mradi huo una dosari nyingi kulingana na
taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ndio msimamizi mkuu wa
benki hapa nchini.
Aliwatoa shaka walimu wote juu ya mchakato wa kuunganishwa kwa mifuko
ya hifadhi ya jamii. Alifafanua kuwa michango yao ipo salama, na mafao
yao watayapata kama kawaida.
Alisema kwamba serikali inatarajia kuunganisha mifuko yote,
inayowahudumia watumishi wa umma na kuwa mfuko mmoja; na wafanyakazi wa
sekta binafsi, wataunganishwa katika mfuko mmoja ili kuongeza tija.
Mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo sasa ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi
ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa
Pensheni wa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Pesheni wa
Watumishi wa Umma (PSPF) na Mfuko wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali
Kuu (GEPF).
Mifuko miwli inayotarajiwa kubakia baada ya marekebisho
yatakayofanyika mwakani ni NSSF kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta
binafsi na PSPF kwa ajili ya watumishi wa umma. Rais alitoa mewito kwa
CWT kutojiingiza katika masuala ya kisiasa, badala yake ijikite
kupigania maslahi na ustawi wa walimu na kusimamia wajibu wa walimu.
“Kuna wakati hiki chama cha walimu kiligeuzwa kama chama cha siasa,
msikubali kwenda kwa mwelekeo huo, hiki ni chombo muhimu, ni lazima
kiende katika mwelekeo mzuri wenye manufaa, na mimi nataka
kuwahakikishia kuwa nawapenda sana walimu, mimi mwenyewe nilikuwa
mwalimu, nafahamu kila kitu kuhusu Ualimu,” alisisitiza Rais Magufuli.
Alitaka pia CWT ijiepushe na vitendo vya rushwa katika uchaguzi.
Alionya kuwa vyombo vya dola vipo macho, kufuatilia na kuchukua hatua
dhidi ya wote wanaojihusisha na rushwa. Kuhusu uhaba wa walimu wa masomo
ya sayansi, Rais Magufuli alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za
kukabiliana na changamoto hiyo.
Alionya kuwa walimu ambao wamekuwa wakikataa kuripoti katika vituo
vya kazi wanavyopangiwa na serikali, itawafuta kazi. Wakati huo huo,
Rais Magufuli aliendesha harambee ya kuchangisha fedha na kufanikiwa
kukusanya Sh milioni 60 za papo kwa papo, ambazo wajumbe wa mkutano huo
pamoja na wanafunzi walioalikwa, watagawiwa
No comments