KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Tazara, Patrick Byatao amesema
wafanyakazi wasio waaminifu wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia
(Tazara) wanalisababishia hasara shirika hilo kutokana wizi wa mafuta
katika treni.
Akizungumza katika hafla ya kuwapa zawadi wafanyakazi bora 10 wa
mwaka 2017, Dar es Salaam jana, Kamanda Byatao aliyataja maeneo korofi
ambayo wizi huo hufanyika kuwa ni pamoja na stesheni ya Mlimba
(Kilombero), Makambako (Njombe), Kongaga (Mbarali), Mpemba (Songwe) na
Tunduma.
Alisema watumishi hao hususani madereva wamekuwa wakishirikiana na
wananchi kuiba mafuta na ndiyo maana shirika hilo haliendelei. Kamanda
Byatao alisema kuwa Oktoba 7, mwaka huu, walifanikiwa kumkamata dereva
wa treni, Kagwa Ruoga na Mathew Mkula ambao walikuwa wakiendesha treni
lililobeba shaba kutoka Zambia kwenda Dar es Salaam na kwamba huku treni
hilo likiwa linatembea waliingiza watu watano na kuanza kuchukua mafuta
ya dizeli.
Aliwataka wananchi kutoshiriki katika matukio hayo ya uhalifu na
kwamba watumishi hao watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuhujumu
uchumi. Aidha, aliwataka askari hao kufanya kazi kwa uadilifu na kuwa
wadadisi ili kugundua matukio mbalimbali ambayo yanaweza kuhatarisha
maisha.
Mmoja wa askari waliopata zawadi, Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Tazara,
Insepkta Halid Kingazi alisema kuwa wataendelea kupambana na uhalifu
ili kuhakikisha wizi unaofanywa unaisha na shirika kubaki salama.
Kingazi alisema kuwa waendesha mashitaka wanapaswa kuwapa ushirikiano
kwa kuhakikisha kesi wanazozipeleka mahakamani zinakwisha kwa wakati.
Kikosi hicho kimetoa zawadi kwa askari wake walipo makao makuu Tazara,
Kituo cha Mlimba Kilombero na Iyunga Mbeya ambapo treni hiyo inapita.
No comments