MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amewataka wakandarasi wataojenga
hospitali au vituo vya afya kwenye wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha
kuhakikisha wanachora ramani ya ghorofa zaidi ya tano ili kutatua
changamoto za uhaba wa maeneo.
Gambo aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa hospitali
ya wilaya ya Arusha katika Kata ya Engutoto, wilayani Arusha. Alisema
kutokana na ukosefu wa ardhi ni vyema sasa wakandarasi kwa kushirikiana
na wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali na wataalamu kuchora ramani ya
ghorofa tano badala ya ghorofa moja.
Gambo alisema lengo la kuwa na ghorofa hizo ni kuondoa tatizo la
uhaba wa ardhi na kusisitiza kuwa Mkoa wa Arusha umejipanga kuhakikisha
kila wilaya inakuwa na hospitali ya wilaya na vituo vya afya ili kuondoa
tatizo la upatikanaji wa huduma za afya.
“Nasisitiza kuwa Mkoa wa Arusha, ujenzi wa hospitali za wilaya lazima
iwepo ramani ya ghorofa tano na kuendelea hata kama mtakwama fedha
mtajenga kidogokidogo kwa sababu ya uhaba wa ardhi,” alisema.
Awali Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha, Dk Simon Chacha alisema wananchi
zaidi ya 80,000 wanatarajia kupata huduma za afya katika Hospitali ya
Wilaya inayojengwa kwenye Kata ya Engutoto eneo la Block “D” lililopo
Njiro Jijini Arusha.
Chacha alisema ujenzi huo wa hospitali ya wilaya utasaidia kupunguza
msongamano wa wagonjwa kwenye vituo mbalimbali vya afya vilivyopo Jijini
Arusha na kuongeza kuwa mradi huo wa uwekaji wa jiwe la msingi ulianza
kutekelezwa Desemba 5 mwaka huu na unatarajia kukamilika katika kipindi
cha miezi saba.
No comments