SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema kuanzishwa kwa chanzo
kingine cha umeme wa maji cha Stiegler’s Gorge, kutazidi kuifanya nchi
iwe na umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.
Aidha, serikali imepongezwa kwa kuwa mstari wa mbele kusisitiza
utunzaji wa vyanzo vya maji. Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco
anayeshughulikia Uzalishaji wa Umeme, Abdallah Ikwasa ametoa kauli hizo
kwenye mtambo wa kufua umeme wa Kidatu wilayani Kilombero mkoani
Morogoro juzi.
Ikwasa alisema kuanzishwa kwa mradi wa Stiegler’s Gorge, kutasaidia
kuboresha upatikanaji wa umeme wa gharama nafuu na rahisi, hivyo
kusaidia ukuzaji uchumi. “Kwa mradi huu wa Stiegler’s Gorge kitakuwa
chanzo kingine cha umeme wa uhakika na utazidi kuufanya umeme
unaozalishwa kwa nguvu ya maji kuendelea kuwa rahisi,” alisema Ikwasa.
Mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge katika maporomoko ya Mto Rufiji,
unatarajiwa kutoa megawati 2,100 na tayari zabuni zimefunguliwa na
kampuni kadhaa zimeshatuma maombi.
Bosi huyo wa Tanesco alieleza kuwa kwa sasa vituo vya kufua umeme kwa
kutumia maji, vinatoa megawati 561 na umeme unaozalishwa nchini
umefikia megawati 1,060. Alieleza kuwa katika kiwango hicho, vituo vya
Tanesco vinazalisha zaidi ya megawati 1,000 na umeme huo unatosheleza
mahitaji ya nchi na kuongeza kuwa katika vituo vya kufua umeme kwa
kutumia maji zipo changamoto kadhaa lakini wanaendelea kuzitafutia
ufumbuzi.
Aliitaja changamoto kubwa ni uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji,
ambako kuna uharibifu wa kingo za mito kutokana na shughuli za kilimo,
ambacho pia kinasababisha udongo kuingia mtoni na hivyo kupunguza kina
cha mito.
Ikwasa alisema moja ya kitu wanachofanya ni kufuatilia miundombinu
ili kuwa na matumizi bora na endelevu ya maji, ili maji yatumike kwa
kazi zote mbili za kilimo na kufua umeme.
“Tutaendelea kuhakikisha kuwa maji yanapatikana na kuendelea kutoa
huduma kwa wananchi ili umeme wa maji uendelee kubaki kuwa wa bei
nafuu,” alisema Ikwasa. Vituo vya Tanesco vya kufua umeme kwa njia ya
maji ni Hale na New Pangani Falls vya mkoani Tanga, Nyumba ya Mungu
mkoani Kilimanjaro, Mtera cha Dodoma na Kidatu na Kihansi vya mkoani
Morogoro.
No comments