Siku chache baada ya Baraza la Magavana nchini Kenya kuunda Kamati ya
Watu 10, kuongoza mazungumzo ya usuluhishi ili kumaliza mgogoro wa
kisiasa unaoendelea nchini humo, Rais Uhuru Kenyatta amesema yupo tayari
kukutana na kuzungumza na Raila Odinga, lakini si kwa mambo ya siasa.
Kenyatta amesema mwishoni mwa wiki kuwa, muda wa siasa umekwisha, na
kwamba, Wakenya wanasubiri maendeleo na si mazungumzo yasiyokwisha ya
mambo ya siasa. Alitoa msimamo huo katika Shule ya Msingi Kinyona Kaunti
ya Muranga wakati wa mazishi ya Susan Chege, ambaye ni mama mzazi wa
mwakilishi wa wanawake Muranga, Sabina Chege.
Amesema, yupo tayari kuzungumza kuhusu namna ya kuwaendeleza Wakenya
na si vinginevyo, hivyo wapinzani wasubiri awamu nyingine ya siasa
wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2022 watakapochuana na mgombea
urais mtarajiwa wa chama cha Jubilee, Naibu Rais wa sasa, William Ruto.
Odinga, Kiongozi wa Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA), anadai
hamtambui Uhuru Kenyatta kuwa ni Rais halali. NASA inaundwa na vyama vya
The Orange Democratic Movement (ODM), Wiper Democratic Movement-Kenya
(WDM-K), Amani National Congress (ANC) na Forum For the Restoration of
Democracy- Kenya (FORD-K).
Viongozi wakuu wa muungano huo ni Raila Odinga, Kalonzo Musyoka,
Musalia Mudavadi, na Moses Wetangula. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka
(IEBC), ilimtangaza Kenyatta kuwa ni mshindi wa uchaguzi wa marudio
uliofanyika Oktoba 26, aliapishwa Novemba 28 kwenye uwanja wa Kasarani
jijini Nairobi.
NASA walitangaza kuwa Odinga angeapishwa siku hiyohiyo kuwa Rais wa
watu lakini mpango huo ulisitishwa. Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa
Waziri Mkuu, akatangaza angeapishwa leo, lakini pia kambi yake
imetangaza kuahirisha hadi hapo itakapotangazwa tena.
Wajumbe wa kamati ya usuluhishi ni Gavana wa Turkana, Josephat Nanok
ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Magavana hao, Gavana wa Siaya Cornell
Rasanga, Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana na Gavana wa Kakamega,
Wycliffe Oparanya.
Wajumbe wengine ni Gavana wa Bomet Joyce Laboso, Gavana wa Uasin
Gishu, Jackson Mandago, Gavana wa Kitui, Charity Ngilu, Gavana wa
Nyandarua, Francis Kimemia, Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi na Gavana wa
Kwale, Salim Mvurya.
Kwenye mkutano wao jijini Nairobi, magavana hao walisema kamati hiyo
itafanya kazi ya kuzipatanisha pande zinazopingana na ‘kuiponya’ nchi
kutokana na mgawanyiko uliojitokeza wakati wa uchaguzi.
Kati ya Agosti na Oktoba mwaka huu, Kenya imefanya uchaguzi wa Rais
mara mbili. Kwanza, Wakenya walipiga kura Agosti 8, mwaka huu na IEBC
ilimtangaza Kenyatta mshindi, NASA wakapinga mahakamani, na Septemba
Mosi Mahakama ya Juu zaidi ikabatilisha matokeo hayo na kuamuru uchaguzi
mwingine ufanyike ndani ya siku 60.
Wakenya walipiga kura tena Oktoba 26, IEBC ikamtangaza Kenyatta
mshindi. Odinga alitangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo ingawa jina lake
lilikuwa miongoni mwa wagombea wanane.
Magavana wanasema umefika wakati kwa viongozi wenye mapenzi mema
kutekeleza kwa vitendo azma ya kupunguza joto la kisiasa ili nchi iwe na
umoja. “Tunaamini kwamba kuna haja kwa sisi magavana kujitolea kuwa
nyenzo ya amani nchini kwa kuzingatia hali ya kisiasa ilivyo sasa.
Kwa nafasi yetu sisi ni viongozi na kwa hiyo tunatoa mwito kwa
viongozi wote kuungana na kutafuta njia ya kupooza joto la siasa,”
alisema Gavana Nanok. Magavana waliwataka viongozi kuacha ajenda zisizo
na tija, na badala yake wazingatie maendeleo ya taifa hilo.
Muda mfupi baada ya kupiga kura kwenye kituo kilichopo katika Shule
ya Msingi Mutomo, Jimbo la Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu Oktoba 26
mwaka huu, Kenyatta alisema, baada ya uchaguzi anaweza kuzungumza na
Odinga ili kuondoa mgawanyiko nchini humo.
Mwanasiasa huyo aliyegombea urais kupitia chama cha Jubilee alikiri
kuwa, Kenya imegawanyika kwa misingi ya ukabila. “Kama kiongozi
unayewajibika lazima umtafute na hilo ndiyo lengo langu,” alisema
Kenyatta.
“Kama nchi lazima tupambane na ukabila kwa kuwa hatuwezi kufanikiwa
kwenye malengo yetu kama tunaendelea na ukabila,” alisema Kenyatta.
Wakati wa kampeni, Kenyatta alisema hakuwa tayari kujadiliana na Odinga
na pia alikataa kusuluhishwa na mtu kutoka nje ya nchi hiyo kwa maelezo
kuwa nchi hiyo haina mgogoro wa kisiasa.
Siku hiyo hiyo ya uchaguzi Spika wa Bunge la Kenya, Justin Muturi
alisema, mamlaka hiyo ipo tayari kusimamia mazungumzo kuwasuluhisha
Kenyatta na Odinga. Muturi alimuonya Odinga afanye mambo yake kwa
kuzingatia sheria na kwamba, Serikali haitaona vema kujadiliana na NASA
ambayo inabadili mwelekeo wake na kuwa kitu kinachoendeshwa kinyume cha
sheria.
Alisema, kama NASA wanaamua kuwa wapiganaji wa msituni serikali
itapambana nao. Odinga alisema, anaweza kujadiliana na Kenyatta kama
majadiliano hayo yatakuwa kwa ajili ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine,
unaoaminika ndani ya siku 90 (tangu Oktoba 26 mwaka huu).
Alisema wakati akihojiwa na kituo cha television cha CNN cha Marekani
kuwa, hata kama Kenyatta akitangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika
Oktoba 26, haitakuwa rahisi kwake kuingoza nchi hiyo.
Alisema, wataipinga Serikali kwa amani, na kwamba, kinaanzishwa
kikundi kingine ndani ya Nasa kiitwacho National Resistance Movement.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, wataipinga serikali kwa amani, si kwa
maandamano. Odinga amekataa ushauri wa Wamarekani kumwelekeza cha
kufanya.
No comments