Serikali imetaka Umoja wa Mataifa (UN) kufanya uchunguzi wa kina na kwa
haraka kubaini waliohusika katika shambulizi kwa askari wa Tanzania
waliokuwa wakilinda amani Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari 14 waliofariki katika
mapigano na waasi wa kikundi cha ADF nchini DRC, Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa amesema Serikali inataka baada ya uchunguzi huo hatua
zichukuliwe ili kutenda haki.
Miili ya askari hao imeagwa leo Alhamisi, Desemba 14,2017 katika viwanja
vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa jijini Dar es Salaam.
“Serikali ya Tanzania inataka Umoja wa Mataifa ufanye uchunguzi wa kina,
ulio wazi na wa ukweli kwa damu hizi za Watanzania zilizomwagika ili
tujue na haki iweze kutendeka. Ni matumaini yetu kuwa Umoja wa Mataifa
watafanya hivyo kwa haraka,” amesema.
Majaliwa ameishukuru Serikali ya DRC na UN kwa ushirikiano baada ya
kutokea shambulizi hilo. Amewataka Watanzania waungane kuwaombea
mashujaa hao na kuenzi mchango wao kwa Taifa.
Amesema Tanzania imekuwa ikishiriki ulinzi wa amani sehemu nyingi kama
vile Lebanon, Darfur na DRC na maeneo yote wanapokuwepo askari wa
Tanzania wanasifiwa kwa ufanisi wa kazi.
“Msiba huu ni wa Taifa lote na watu wote wenye kupenda amani, daima
tutawakumbuka mashujaa wetu na kuendelea kuenzi na kujivunia kazi zao na
mchango wao mkubwa kwa nchi yetu na duniani kwa jumla,” amesema.
Waziri Mkuu Majaliwa ameliambia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
kwamba, yaliyotokea DRC yasiwakatishe tamaa katika kutimiza wajibu wao
nchini humo na kwingineko ambako wanatekeleza majukumu yao ya ulinzi wa
amani.
Awali, akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari hao, Mkuu wa Majeshi
ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo alisema askari hao waliuawa kwenye
mapigano yaliyodumu kwa saa 13.
Amesema majeruhi wa shambulio hilo linalodaiwa kufanya na waasi wa ADF
wanaendelea vizuri na wanapatiwa matibabu katika hospitali zilizopo
Goma, Kinshasa na wengine wamepelekwa Uganda.
Shughuli ya kuaga miili ya mashujaa hao imehudhuriwa na viongozi kadhaa
wakiwemo, Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mkewe Salma; wakuu wa majeshi
wastaafu Robert Mboma, Mirisho Sarakikya na Davis Mwamunyange; Waziri
Mkuu mstaafu Mizengo Pinda; mawaziri, wabunge na wawakilishi wa Umoja wa
Mataifa.
Miili ya askari hao ilirejeshwa nchini kwa ndege ya Umoja wa Mataifa Desemba 11,2017.
Jumapili Desemba 10, 2017 Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James
Mwakibolwa alisema askari hao walivamiwa kambini na waasi wa ADF na
mapigano yalidumu kwa takriban saa 13. Alisema askari 14 wa JWTZ
waliuawa, 44 walijeruhiwa na wengine wawili hawajulikani walipo.
Taarifa iliyotolewa baadaye na jeshi ilisema askari mmoja amepatikana.
Mwakibolwa alisema tukio hilo lililotokea Desemba 7,2017 katika kambi
ndogo iliyopo katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa
Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu nchini DRC.
No comments