MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) imefafanua kuhusu viwango vya kodi, anavyopaswa kukatwa mtu binafsi aliyeajiriwa.
Akizungumza kwenye kipindi cha ‘Kodi kwa Maendeleo’ kinachorushwa na
Shirika la Utangazaji nchini (TBC1) wiki hii, Meneja wa Huduma na Elimu
kwa Mlipa Kodi wa TRA Makao Makuu, Gabriel Mwangosi alisema kuwa mwajiri
atakata kodi, pale tu ambapo mfanyakazi au mwajiriwa anapata mshahara,
kipato au ujira.
Mwangosi alisema kiwango cha kodi, ambacho mtu anatakiwa kukatwa kwa
mujibu wa sheria ya kodi ya mapato, vinatofautiana kutoka mtu mmoja hadi
mwingine, kulingana na kiwango cha kipato anachopata mtu kwa mwezi.
Akifafanua kuhusu kodi ya ajira, ambayo mwajiriwa anakatwa kwenye
mapato au mafao yake, Mwangosi alisema kuwa kiwango cha mshahara au
kipato au ujira, kinachotakiwa kukatwa kodi ni kile kinachozidi Sh
170,000 kwa mwezi.
Alisema kwa kuwa kwenye ajira kuna vyanzo tofauti tofauti vya mapato
kwa mwajiriwa, kama vile motisha (bonus), kamisheni, ujira, mshahara,
malipo ya likizo, posho na mengineyo, ambayo yote yakijumlishwa
yanatengeneza kipato cha mwezi, hivyo kipato hicho kama hakizidi Sh
170,000 hakikatwi kodi.
“Kipato cha Shilingi 170,000 kushuka chini hakina kodi, kimesamehewa
kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato Kifungu namba 10 ukisoma pamoja
na jedwali la pili la kodi ya mapato ambalo linaonesha viwango
vilivyosamehewa kodi kuwa ni pamoja na hiki cha Sh 170,000 kushuka
chini,” alieleza Mwangosi.
Kwa mujibu wa Meneja huyo wa TRA, kiwango kinachozidi Sh 170,000
lakini hakizidi Sh 360,000 kwa mwezi, kodi yake ni asilimia tisa.
Alisema kwa mfano mtu analipwa Sh 360,000 au 240,000, kinachofanyika ni
kwamba inatolewa Sh 170,000 kwenye kipato hicho na kiasi kinachobaki
ndiyo kinakatwa kodi ya asilimia tisa.
TRA inasema kuwa kwa mwajiriwa anayepata kipato kinachozidi Sh
360,000 lakini hakizidi Sh 540,000 kwa mwezi, kodi yake ni Sh 17,100,
lakini inajumlishwa na asilimia 20 ya kodi kwa kipato kinachozidi Sh
360,000.
Vivyo hivyo kwa kipato kinachozidi Sh 540,000 lakini hakizidi Sh
720,000 kwa mwezi, kodi yake ni Sh 53,100, lakini itaongezwa na asilimia
25 ya kiwango kinachozidi Sh 540,000.
“Kiwango chochote cha kipato cha kuanzia Sh 720,000 kwenda juu kwa
mwezi, kodi yake ni Sh 98,100, lakini inajumlishwa na asilimia 30 ya
kiwango kinachozidi Sh 720,000, hivyo kodi kwa mtu binafsi hata kama
analipwa Sh milioni 20 au zaidi, anakatwa kodi kwa utaratibu huu,”
alisema Mwangosi.
Alisema kiwango hicho cha kodi cha asilimia 30 kwa mujibu wa sheria
za kodi ya mapato, ndiyo kiwango cha juu zaidi kuliko kiwango kingine
chochote. Alisema kwenye kodi kuna viwango vya asilimia tano, asilimia
10, asilimia 15, asilimia 20, asilimia 25 na asilimia 30 ambacho ndiyo
kiwango cha mwisho kwenye kodi ya mapato.
Mwangosi alisema kuwa mfumo wa kodi ya ajira, unamtaka mwajiriwa
alipe kodi kadri anavyopata kipato (PAYE). Alisema mwajiriwa anayepata
kipato kidogo, pia analipa kodi kidogo na anayepata kipato kikubwa na
kodi pia huwa kubwa.
Punguzo la kodi Kwa mujibu wa Mwangosi, Serikali kila mara imekuwa
ikirejea viwango vya kodi na kuendelea kuvipunguza ili kuongeza watu
wengi zaidi kwenye wigo wa kodi.
Alisema viwango vya kodi vinapokuwa juu sana, vinawafanya watu
kukwepa kodi na ndiyo maana Serikali huvirejea viwango hivyo kila mara.
Alisema kwa zamani asilimia ya kodi ya ajira ilikuwa kubwa, kwa kuwa
ilianzia asilimia 17 baadaye ikashushwa hadi asilimia 15, ikashushwa
tena hadi asilimia 14, baadaye asilimia 12 na 11, na sasa ni asilimia
tisa.
Mwangosi alisema kuwa matokeo ya punguzo la asilimia tisa la kodi ya
ajira, alilolitoa Rais John Magufuli, linaonekana zaidi kwa watu wenye
kipato cha chini, tofauti na wenye kipato kikubwa.
No comments