WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema hakuna mgawo wa umeme
nchini na kwamba tatizo la kukatika kwa umeme linalojitokeza maeneo
mengi hivi sasa litamalizika Desemba 15, mwaka huu.
Aidha amesema tatizo hilo linatokana na kufanyika kwa marekebisho ya
mitambo iliyochakaa kwa kudumu kwa takribani miaka 40 sasa. Akizungumza
katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Televisheni ya Taifa
(TBC 1), Dk Kalemani alisema lengo la marekebisho yanayofanywa ni
kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mitambo itakayowezesha upatikanaji wa
umeme wa uhakika wakati wote.
Alisema umeme una umuhimu katika Taifa lolote likiwemo Tanzania
ambalo linapambana kwenda katika uchumi wa kati wa viwanda na kusisitiza
kuwa wakati wa utekelezaji wa hatua hiyo ya maendeleo ni vigumu
kutenganisha na maendeleo ya nishati.
“Tuna upungufu wa umeme kutokana na ukarabati unaoendelea, mafundi
hawalali kuhakikisha hali inakuwa sawa, hadi kufikia Desemba 15, mwaka
huu tutakuwa tumefanya ukarabati katika sehemu kubwa na kutakuwa na
tofauti kubwa,” alisema Dk Kalemani.
Aidha akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa mtambo wa uzalishaji umeme
wa Kinyerezi 2 jijini Dar es Salaam, Waziri huyo alisema hadi sasa
ujenzi wake umeshakamilika kwa asilimia 86 na kwamba kuanzia mwezi huu
megawati 30 zitaanza kuzalishwa kila mwezi.
Alisema pia wanaendelea na mchakato wa kumpata mkandarasi
atakayejenga mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge, uliopo katika
maporomoko ya maji ya Mto Rufiji unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,100
kwa mkupuo.
Kwa mujibu wa Waziri Kalemani matarajio ni kuwa hadi kufikia Januari
au Februari mwakani, mkandarasi huyo atakuwa amepatikana na aliwataka
wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi cha maboresho yanayoendelea.
Mbali na miradi hiyo, Dk Kalemani pia alisema mradi wa umeme wa
Makambako- Songea ni moja ya miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa na
utakamilika ifikapo Septemba, mwakani na utakuwa na vituo vitatu vya
kupozea umeme.
Alisema hatua hiyo na nyinginezo za utekelezaji wa mpango wa
usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa REA III umelenga
kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2021
huku hivi sasa vijiji takribani 7,000 havijaunganishwa na huduma hiyo
No comments