SERIKALI imewataka walimu wapya 3,033 wa shule za msingi na
sekondari, kuripoti katika vituo vya kazi kuanzia Desemba 27, mwaka huu
hadi Januari 7.
Kati ya walimu hao, walimu 266 ni wa sekondari na walimu 2,767 ni
shule za msingi. Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo alipokuwa akitoa
taarifa ya ajira mpya kwa walimu wa msingi na sekondari.
Alikuwa akitangaza nafasi za ajira kwa walimu 3,033 wa shule hizo,
watakaoziba nafasi zilizoachwa wazi na walimu waliondolewa kwenye
utumishi wa umma baada ya kubainisha kuwa na vyeti vya kugushi.
Alionya kuwa walimu watakaobainika kuchukua posho ya kujikimu na
baadaye kuondoka kwenye vituo vyao vya kazi na ikibainika, watachukuliwa
hatua kwa mujibu wa sheria. “ Walimu hawa wanatakiwa kuripoti katika
vituo vya kazi kuanzia Desemba 27 mwaka huu hadi Januari 7 mwakani,
wakiwa na vyeti vya kidato cha nne na sita, vyeti vya taaluma vya
kuhitimu mafunzo ya ualimu kwa ngazi husika na cheti cha kuzaliwa.
Walimu wanaoajiriwa, watatakiwa kuripoti katika ofisi za wakurugenzi
wa halmashauri zilipo shule walizopangiwa na kisha watakwenda kuripoti
kwenye shule husika...vituo vyao vya kazi ni shule za msingi na
sekondari kwa waliopangiwa kufundisha elimu ya msingi au sekondari na si
makao makuu ya halmashauri,” alisema.
Jafo aliongeza kuwa, “ kila mwalimu amepangiwa kwenye shule ambayo
haina walimu wa somo husika au kuna upungufu mkubwa shuleni.” Alisema
waajiriwa wapya, hawatahamishwa kutoka shule moja kwenda shule nyingine,
ndani au nje ya halmashauri au mkoa, bila ridhaa ya ofisi ya Rais
Tamisemi.
“Nachukuwa fursa hii kuwataka wakurugenzi katika halmashauri ambazo
walimu hawa wataripoti, kuwapokea walimu hao kwa kuzingatia taratibu na
kanuni za utumishi wa umma na baadaye kutoa taarifa ya kuripoti kwao,”
alisema waziri huyo.
No comments