WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewatoa hofu wakazi 1,000 wa Manispaa ya
Songea, wanaoidai fidia ya Sh bilioni 3.8 ya eneo lao, ambalo
limechukuliwa na kuwa eneo la kiuchumi mkoani Ruvuma (Ruvuma SEZ) kwa
ajili ya ujenzi wa viwanda.
Alitoa ahadi hiyo jana wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya
Mwengemshindo katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye Manispaa
hiyo. Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano, inatambua kilio
chao ambacho, alisema ni cha muda mrefu na kwamba alishawahi kupata ombi
maalumu kutoka kwa Mbunge wao wa zamani, Leonidas Gama ambaye sasa ni
marehemu.
“Alipotoka kutibiwa India alikuja ofisini kwangu na kunieleza kwamba
ana mambo mawili ambayo nikifanya ziara mkoani Ruvuma anaomba
niyatafutie ufumbuzi. La kwanza lilikuwa ni hili la fidia kwa wakazi wa
Mwengemshindo na la pili lilikuwa ni la ujenzi wa kituo cha mabasi cha
mjini Songea,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Leo nimefanya ziara maalumu kwa ajili yenu kwa
sababu serikali ya awamu ya tano iko kwa ajili yenu na hasa wananchi
wanyonge. Na tatizo hili nalijua, kabla sijafika hapa, nilipita kwenye
eneo husika na ofisa mipango miji akanionesha ramani ya eneo lenu hili”.
Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba eneo hilo limetengwa na
Manispaa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, ambapo wawekezaji watatu tayari
wamekwishajitokeza na wanataka kujenga viwanda vitatu. “Kutakuwa na
kiwanda cha kusindika mahindi, kutengeneza pumba za kuku na ng’ombe na
mbolea.
Kiwanda cha pili kitakuwa ni cha kusindika kahawa na cha tatu
kitakuwa ni cha kukamua mafuta ya mbegumbegu,” alisema na kuongeza
kwamba reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbaba Bay inatarajiwa kupita kwenye
eneo hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kuchelewa kwa malipo yao, Waziri Mkuu alisema
kwamba kati ya wawekezaji hao watatu aliyekwishalipa fidia ni mmoja tu
na kwamba kwa mujibu wa sheria ya uwekezaji, fidia inapaswa kulipwa na
mnunuzi wa eneo husika.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alikiri kuwepo kwa mapungufu wakati wa
ulipaji kwa sababu walifuata orodha ya majina (kialfabeti) badala ya
kutoa malipo kwa wakazi wa eneo husika. “Sasa hivi mwekezaji anataka
kuanza ujenzi, lakini ndani ya eneo lake kuna watu ambao bado
hawajalipwa, kwa hiyo hawawezi kutoka hadi wale waliobakia nao walipwe.
Serikali itawafuatilia hawa wawekezaji wengine ili nao walipe fedha
zao haraka ili waliobakia waweze kulipwa,” alisema. Jumla ya watu 2,179
walifanyiwa uthamini mwaka 2008 na gharama yao kubainika kuwa ni Sh
3,254,737,622.
Kuanzia Juni 8-19, 2015, Serikali iliwalipa wakazi 1,179 Sh
1,920,242,121 ambapo kati ya hizo, Sh 1,210,078,261 zilikuwa ni malipo
ya thamani ya mali za wananchi na Sh 710,163,860 zilikuwa ni riba
kutokana na malipo hayo kuchelewa kufanyika.
Eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2,033 (sawa na ekari 5,000),
lilitwaliwa na Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) kwa
kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Ruvuma na Manispaa ya Songea tangu
mwaka 2007.
Eneo hilo linajumuisha mitaa ya Luwawasi (Mkuzo), Mwengemshindo na
Luhira. Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemuagiza Ofisa Ardhi wa Manispaa ya
Songea, Kundaeli Ndemfoo afuatilie suala la Monica Miti na wanawe ambao
walidhulumiwa nyumba ya urithi na aliyekuwa mwanasheria wa manispaa
hiyo.
Alitoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata
ya Mwengemshindo baada ya kupokea bango lililoandikwa na Monica kuomba
arejeshewe umiliki wa nyumba ya marehemu muwewe.
Alipopewa nafasi ya kueleza tatizo lake, Monica Miti ambaye alimtaja
mwanasheria huyo kwa jina moja Mwakasungura, alidai kuwa mwanasheria
huyo alighushi hati ya nyumba, na kuwatoa ndani ya nyumba yeye na watoto
wa marehemu
No comments