Heade

JAJI MKUU;KUSHINDA AMA KUSHINDWA YOTE NI HAKI

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma amesema siyo sahihi mtu kufi kiri ili vyombo vya sheria hususani Mahakama ionekane imetenda haki, lazima ashinde kesi.
Amesema, msingi bora wa haki ni pamoja na wahusika kupata suluhu nje ya mahakama. Jaji Mkuu Juma alisema hayo jana wakati akifungua Wiki ya Utoaji wa Elimu ya Sheria katika maadhimisho yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Kilele cha Maadhimisho haya kitafanyika Februari 1, 2018 kikiongozwa na Rais John Magufuli katika Viwanja vya Mahakama vilivyopo Mtaa wa Chimala, Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni, “Matumizi ya Tehama Katika Utoaji wa Haki kwa Wakati na kwa Kuzingatia Maadili.”
Ufunguzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sheria wakiwamo majaji, wasajili wa mahakama, mahakimu, mawakili na watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria. “Mahakamani siyo lazima ushinde…
Wengine wanadhani ili haki itendeke, ni lazima wao wawe wameshinda. Haki siyo ushindi, bali ni mchakato mzima wa kufungua mashauri, kuendesha kesi, kutoa hukumu na kukata rufaa pale inapohitajika kama upande mmoja haukuridhika,” alisema Jaji Mkuu.
Alisema katika kuhakikisha haki za kisheria zinawafikia wananchi, Mahakama ya Tanzania imeanza mchakato wa kuendesha mahakama inayotembea (gari maalumu la kimahakama). “Mahakama sasa inawafuata wananchi kwa gari maalumu na kupitia Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano),” alisema.
Akizungumzia baada ya ufunguzi kuhusu mahakama inayotembea, Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi alisema ni hatua kubwa katika kuifanya Mahakama iwe karibu na wananchi kwani itawafuata sehemu mbalimbali zikiwamo za vijijini kuwawezesha wengi kupata haki stahiki kwa wakati muafaka.
Awali Jaji Mkuu Juma aliwataka wananchi ambao ni kati ya wadau wa Mahakama katika utoaji haki, kuepuka kulalamika wanapoona haki haitendeki bali wawe jasiri kuchukua hatua haraka kuzijulisha mamlaka zinazohusika.
“Ukiona rushwa au mazingira ya rushwa, usilalamike; chukua hatua hata kwa kuwajulisha PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa- Takukuru) maana kulalamika bila kuchukua hatua hakusaidii kumaliza tatizo, bali kumtaja asiye na maadili ili tuachane naye,” alisema Jaji Mkuu.
Aliwataka wananchi kutumia nguvu na nafasi zote kujifunza ili kuelewa taratibu za mashauri katika mahakama nchini akisema likifanyika, litaondoa uwezekano wa watu kupoteza haki zao kwa kutokujua taratibu zake za kisheria.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu huyo, watu wengi wanapoteza muda kwa kutafuta haki zao katika maeneo yasiyohusika na utoaji haki za kisheria. “Wengi wanapoona hawapati haki wanapoteza muda kuzunguka kwenye ofisi mbalimbali zikiwamo za viongozi wa Serikali, badala ya kukataa rufaa… Tehama, itasaidia kukufanya ujue hatua za shauri lako; ujue liko wapi, limefikia hatua gani na kama linakwamishwa, linakwamishwa wapi,” alisema Jaji Mkuu.

No comments

Powered by Blogger.